Kisii:Mwanafunzi wa chuo akamatwa kwa kuendesha duka feki la Jumia, kulaghai watu mamilioni

Mwanafunzi huyo wa mwaka wa 3 chuo cha Kisii na wenzake kutoka Kiambu walikuwa wanaendesha biashara feki wakiiga duka la mitandaoni la Jumia.

Muhtasari

• DCI walisema kuwa mwanafunzi huyo na wenzake walikuwa wanauza bidhaa hewa kwa ofa ya Krismasi na mwaka mpya.

Mlaghai huyo alikuwa anaendesha ukurasa feki wa Jumia
Mlaghai huyo alikuwa anaendesha ukurasa feki wa Jumia
Image: Facebook//DCI

Walaghai watatu mashuhuri walikamatwa mwishoni mwa juma kwa kujipatia pesa kutoka kwa watu kwa njia ya ulaghai, kwa kutumia majukwaa ya uwongo ya mtandaoni yanayodaiwa kuuza bidhaa.

Kulingana na taarifa na kitengo cha ujajusi DCI,  nwatatu hao ni pamoja na Dickson Magembe, Dionicious Omonyi na Derrick Kodek walikamatwa kwa kishindo na maafisa, kufuatia malalamiko mengi yaliyopokelewa kutoka kwa umma kupitia mitandao ya DCI ya Facebook na Twitter.

Watatu hao wanaaminika kujipatia mamilioni ya pesa kutoka kwa wanunuzi ambao hawakutarajia, kwa kuendesha akaunti ghushi wakiiga maduka maarufu ya mtandaoni ya JUMIA.

Kupitia ukurasa ghushi wa Facebook ‘Jumia Shopping’ watatu hao waliendesha promosheni katika kipindi cha Krismasi na Mwaka Mpya ikitoa punguzo la hadi 40% kwa bidhaa mbalimbali za nyumbani, na kuvutia wanunuzi wengi bila kutarajia.

Nambari ya till ya MPESA ambapo amana zingewekwa kabla ya kuwasilisha bidhaa na baada ya malipo kufanikiwa, ankara itatumwa kupitia WhatsApp ikiahidi kutumwa bila malipo ndani ya saa 24.

Hiyo ingeashiria mwisho wa mawasiliano kwani wateja wenye hamu wangeblockiwa kote mitandaoni, na kuwaacha wakiwa wamekata tamaa na hasara kubwa ya kubeba.

DCI waliripoti kuwa walaghai hao walimuibia mtu mmoja kutoka kaunti ya Tharaka Nithi kiasi cha karibia laki moja kabla ya kumzimia simu na kokatisha mawasiliano naye kote mitandaoni.

“Haya yalimtokea mwathiriwa huko Mukothima, Kaunti Ndogo ya Tharaka Kaskazini, ambaye alilipa Sh 95,000 kwa kiti cha viti 7 na meza ya kahawa. Hii ni baada ya ofa kutolewa kwenye ukurasa ghushi wa Facebook ikitangaza punguzo la 40% kwa viti vya kuegemea na vitu vingine vya nyumbani,” DCI waliripoti.

Baada ya kuwatia nguvuni, polisi walipata laini za simu zipatazo 22 ambapo mmoja wa wezi hao ni mwanafunzi wa chuo kikuu cha Kisii akisoma mwaka wa 3.