Seneta Olekina kufungua maduka 3 Narok ili kuwapa vijana ajira

Olekina alisema kuwa maduka hayo yatakuwa na huduma za kusafirisha bidhaa hadi nyumbani kwa wateja, hivyo kuwaajiri vijana wengi.

Muhtasari

Tarehe 1 Februari 2023 maduka matatu ya kwanza yaliyoko Olululunga, Ewaso Nyiro na Talek yatafunguliwa - Olekina.

LEDAMA 2
LEDAMA 2

Seneta wa Narok Ledama Olekina ametangaza mpango wake wa kuwaajiri kazi vijana wa kaunti hiyo kupitia kufungua biashara mbalimbali.

Olekina alisema kuwa kuanzia Februari mosi, atafungua maduka matatu katika maeneo mbalimbali Narok, kama njia moja ya kuwakimu vijana.

 “Tarehe 1 Februari 2023 maduka matatu ya kwanza yaliyoko Olululunga, Ewaso Nyiro na Talek yatafunguliwa. Maduka hayo yatasimamiwa na vijana wa eneo hilo kutoka maeneo hayo na kila duka litaanzisha mfumo wa utoaji wa huduma za nyumbani na kuajiri vijana wasiopungua 10. Tuwekeze kwenye uchumi wetu na tutamaliza ukosefu wa ajira...” Olekina alisema.

Alijilinganisha na mwanzilishi wa maduka ya jumla ya Walmart aliyeanzisha maduka hayo mwaka 1962, na baadae matawi mbalimbali  ambayo yanawasaidia watu.

“Mnamo 1962, Sam Walton alianza na duka moja tu -Walmart -na dhamira moja: kusaidia watu kuokoa pesa ili waweze kuishi vyema. Leo Walmart ina maduka 11,500 yanayoajiri maelfu ya watu. Mnamo 2023 Sen Ledama Olekina alianzisha NarokBiz shirika la biashara la vijana ili kuunda nafasi za kazi kwa vijana wa Kaunti ya Narok na vile vile kukuza bidhaa zinazotengenezwa nchini,” alizidi kusema dhamira yake.

Seneta huyo miezi kadhaa iliyopita alizindua kampuni yake ya kutengeneza bidhaa za mawazi pamoja na maziwa yenyewe kwa jina Enkanasa Cow ambayo amesema amekuwa akisambaza kwa wanajamii hiyo kwa bei nafuu.