Jamii ya wasioamini Mungu Kenya wasikitika kugundua maombi hufanyika ofisini IEBC

Walisema kuwa maombi kufanywa katika ofisi na taasisi za kiserikali ni haramu.

Muhtasari

• Jamii hiyo ilisema kuwepo kwa maombi IEBC kunaenda kinyume na kifungu cha 8 cha katiba.

• Walimtaka mkurugenzi mtendaji kupiga marufuku maombi kufanyika katika ofisi za IEBC.

Rais wa jamii ya wasioamini Mungu
Harrison Mumia Rais wa jamii ya wasioamini Mungu
Image: Instagram

Jamii ya watu wasioamini uwepo wa Mungu nchini Kenya imetoa taarifa ya kushangaa kwao kugundua kuwa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC walikuwa wanaandaa maombi ya ushirika.

Jamii hiyo ikiongozwa na rais wao Harrison Mumia ilisema kuwa kuweka hafla ya maombi ya ushirika kuwa lazima kwa wafanyikazi ni jambo ambalo linaenda kinyume na haki za kimsingi za watu.

“Wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya Tathmini ya Baada ya Uchaguzi - Uchaguzi Mkuu wa Agosti 2022 huko @IEBCKenya, ilikuja kwetu kuwa IEBC kulikuwepo na maombi ya ushirika. Tumemwomba Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa IEBC aondoe maombi ya Shirika kulingana na Kifungu cha 8 cha Katiba yetu,” sehemu ya taarifa yao ilisoma.

Muia alizidi kufafanua kuwa kifungu cha 8 cha katiba ya mwaka 2010 ya Kenya kinapiga marufuku kwa ofisi yoyote ya Serikali kulazimishia maombi ya dini kwa wafanyikazi wake.

Alisema kuwa haikuwa picha nzuri kuona taasisi za kiserikali kama IEBC kuwa na maombi ya ushirika kwa wafanyikazi wake, licha ya kuwa na wengine ambao si Wakrtisto na wengine wakiwa mrengo wa kutoamini uwepo wa Mungu.

Jmii hiyo mwaka jana waliburuzana vikali na aliyekuwa waziri wa elimu George Magoha ambapo walimtaka kuondoa hafla ya maombi shuleni kwa ajili ya watahiniwa, zikiwa zimesalia siku chache kufanyika kwa mitihani ya kitaifa.