Nyeri: Mwalimu aliyejigongelea misumari ndani ya jeneza alifariki kwa kukosa hewa safi

Mwalimu Joseph Githogo alipatikana amejigongelea misumari ndani ya jeneza, kando yake kukiwa na vitu vya kishirikina.

Muhtasari

• Kando ya jeneza lake kulikuwepo pembe la ng'ombe, bendera nyeusi na waraka wenye maandishi yasiyoeleweka.

• Uchunguzi ulibaini kuwa alikuwa amejisulubisha ndani ya jeneza na juu yake kulikuwa na saruji nyepesi.

Mwili wa mwanamke wapatikana umegongelewa misumari
Mwili wa mwanamke wapatikana umegongelewa misumari
Image: Maktaba

Uchunguzi wa mwili wa mwalimu wa Nyeri aliyepatikana amefariki ndani ya nyumba yake akiwa amegongelewa misumari kwenye jeneza lenye muonekano wa boti umebaini kuwa alifariki kwa kukosa hewa safi ya kupumua.

Katika taarifa ya awali ambayo Radio Jambo iliripoti wiki jana, Mwalimu Joseph Githogo aliyekuwa akifunza katika shule ya upili ya Muhoya kaunti ya Nyeri alikuwa ametoweka kwa wiki tatu.

Mara ya mwisho alionekana ilikuwa ni Desemba 22 baada ya kumaliza kusimamia mitihani ya KCSE na hakuweza kuonekana mpaka mwili wake ulipopatikana ndani ya nyumba yake ya kukodisha ukiwa katika hali yenye ukakasi na utatanishi mwingi.

Alipatikana ndani ya jeneza lenye muonekano wa boti akiwa amegongelewa misumari na jeneza hilo lilikuwa limemwagiliwa saruji nyepesi juu yake.

Kulingana na ripoti ya awali, kando ya jeneza hilo kulikuwa na vitu vya utata ikiwemo bendera ndogo ya rangi nyeusi, pembe moja la ng’ombe na waraka wenye maandishi yaliyokuwa yameandikwa kwa lugha ya kigeni ambayo hakuna aliyeweza kuitafsiri.

Kulingana na jarida moja la humu nchini, polisi wamefanikisha uchunguzi wao ambao umeoana na uchunguzi wa maiti ambapo walisema alijisulubisha katika jeneza hilo na kifo kusababishwa kwa kukosa hewa safi ya kupumua.

"Uchunguzi wetu ambao hadi sasa umelingana na uchunguzi wa maiti unaonyesha kuwa alijipachika ndani ya jeneza na kufunga hewa yoyote isiingie au kutoka," alisema kamanda wa polisi.

Akiwa ndani ya jeneza, kamanda wa polisi Bw Mwania alisema mwalimu huyo wa shule ya upili alijifunika kwa ‘leso la Kimasai’ jekundu na karatasi ya polythene. Alikutwa uchi.

Uchunguzi wa maiti ulionyesha zaidi kuwa marehemu hakumeza sumu yoyote wala hakuwa na majeraha yoyote mwilini.