Usain Bolt amepoteza £10.3m kutokana na ulaghai-asema wakili wake

"Tutaenda mahakamani na suala hilo ikiwa pesa hazitarejeshwa," wakili alisema

Muhtasari

•Tume ya Huduma za Kifedha ya Jamaica imeanza uchunguzi dhidi ya kampuni ya uwekezaji, Stocks and Securities Limited (SSL).

•FSC ilisema "inafahamu ripoti za madai ya ulaghai" na kwamba mchakato wa uangalizi utairuhusu kuona uhamishaji wa fedha na dhamana ndani na nje ya kampuni ya SSL.

alishinda medali nane za dhahabu za Olimpiki kabla ya kustaafu mwaka wa 2017
Usain Bolt alishinda medali nane za dhahabu za Olimpiki kabla ya kustaafu mwaka wa 2017
Image: BBC

Bingwa wa Olimpiki Usain Bolt analenga kurejesha zaidi ya $12.7m (£10.2m) ambazo wakili wake anasema amepoteza baada ya kulaghaiwa.

Tume ya Huduma za Kifedha ya Jamaica imeanza uchunguzi dhidi ya kampuni ya uwekezaji, Stocks and Securities Limited (SSL).

Mwanariadha huyo aliyestaafu mwenye umri wa miaka 36 alikuwa na uwekezaji na kampuni ya SSL kwa zaidi ya muongo mmoja.

"Tutaenda mahakamani na suala hilo ikiwa pesa hazitarejeshwa," wakili Linton Gordon alisema.

"Ni jambo la kutamausha sana, na tunatumai kuwa suala hilo litatatuliwa kwa njia ambayo Bw Bolt atarejesha pesa zake na kuweza kuishi kwa amani."

Meneja wa Bolt Nugent Walker aliiambia Jamaica Gleaner kwamba bingwa huyo mara nane wa Olimpiki aligundua kwamba kuna "kasoro".

FSC ilisema "inafahamu ripoti za madai ya ulaghai" na kwamba mchakato wa uangalizi utairuhusu kuona uhamishaji wa fedha na dhamana ndani na nje ya kampuni ya SSL.

"Tume ya Huduma za Kifedha ya Jamaika wakati huo huo itaendelea na uchunguzi wake katika masuala yanayohusiana na SSL," iliongeza.

Kampuni ya SSL ilisema uchunguzi wake wa ndani unaonyesha kuwa mfanyakazi wa zamani ndiye aliyehusika na madai ya udanganyifu na kuongeza kuwa "imelielekeza suala hilo kwa mamlaka husika za kutekeleza sheria".

Bolt alistaafu riadha mwaka wa 2017 baada ya kushinda medali 11 za dhahabu za Ubingwa wa Dunia na medali nane za dhahabu za Olimpiki.

Wakati wa Michezo ya Olimpiki ya Beijing ya 2008, Bolt aliweka rekodi mpya za ulimwengu za mita 100 na 200.

Muda wake wa mita 100 wa sekunde 9.572 unasalia kuwa rekodi ya dunia.