logo

NOW ON AIR

Listen in Live

"Hakuna minisketi,tumbo-cut, skin tight!" Chuo Kikuu cha Eldoret chatoa sheria kali kwa wanafunzi

Wanafunzi pia wameshauriwa kuvaa nguo zinazozingatia jinsia yao.

image
na Samuel Maina

Habari21 January 2023 - 08:56

Muhtasari


  • •Msimamizi wa wanafunzi wa chuo hicho  aliwakumbusha wanafunzi  wote kuhusu mitindo mavazi inayokubalika humo shuleni.
  • •Wanafunzi pia wameshauriwa kuvaa nguo zinazozingatia jinsia yao kama ilivyo kwenye maelezo yao yaliyoandikwa katika rekodi za shule.

Takriban wiki mbili tu baada ya Chuo Kikuu cha Kenya Methodist (KeMU) kutoa miongozo mipya mikali kuhusu mitindo ya mavazi ya wanafunzi, Chuo Kikuu cha Eldoret kimefuata mkondo huo huo.

Katika memo iliyotolewa mnamo Januari 19, msimamizi wa wanafunzi wa chuo hicho kikuu Dkt Lelei K. Kiboiy aliwakumbusha wanafunzi  wote kuhusu mitindo mavazi inayokubalika humo shuleni.

"Wanafunzi wote wanatarajiwa kuvaa mavazi ya kawaida ya heshima, yanayokubalika na yanayofaa ambayo yanawezesha mazingira mazuri ya masomo," memo ambayo ilifikia Radio Jambo ilisoma.

Hatua hiyo ilifuatia baada ya uongozi wa shule kugundua kuwa baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakivalia visivyofaa.

Kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazosimamia maadili na nidhamu ya wanafunzi wa Chuo hicho, nguo kama vile sketi ndogo (micro/mini-skirt), suruali ya kubana ngozi, tumbo-cut na nguo za uwazi zinazoonyesha ndani zinachukuliwa kuwa zisizofaa miongoni mwa wanafunzi wa kike.

Wanafunzi wasichana pia hawaruhusiwi kuvaa jeans zilizochanika au kuraruka, blauzi ama nguo yenye mkato wa chini, kaptula fupi, tshirt zisizo na mikono na mavazi yanayoonyesha mikanda ya sidiria.

Kwa upande wa wanafunzi wanaume, ni marufuku kuvaa mavazi yanayoonyesha kifua na suruali zilizochanika. Pia hawaruhusiwi kuwa na suruali inayolegea.

"Wanafunzi wote wanashauriwa, wakati wote kutovaa mavazi yasiyofaa katika chuo kikuu kwani hii inaweza kuhitaji kuchukuliwa hatua za kinidhamu," memo ilisoma.

Wanafunzi pia wameshauriwa kuvaa nguo zinazozingatia jinsia yao kama ilivyo kwenye maelezo yao yaliyoandikwa katika rekodi za shule.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved