Babu Owino: Kama si Handshake, Raila Odinga angekuwa rais wa Kenya sasa hivi

Binafsi mimi siamini kabisa katika mambo hayo ya handshake - Babu Owino.

Muhtasari

• Mbunge huyo alitetea hatua ya Odinga kuwataka viongozi wa Nyanza kuhudhuria ziara ya rais Ruto.

• Alisema ili kuwe na maendeleo katika nchi yoyote, ni sharti kuwepo na amani.

Babu Owino
Babu Owino
Image: Facebook

Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino amesisitiza msimamo wake kuwa rais mstaafu Uhuru Kenyatta alimcheza kinara wa ODM Raila Odinga katika uchaguzi mkuu wa Agosti mwaka jana.

Aizungumza katika mahojiano ya kipekee na mwanablogu Esther Nyonje, Owino alsiema kuwa kama si yale maridhiano ya Handshake baina ya Odinga na Kenyatta, kiongozi huyo sasa hivi angekuwa ndiye rais wa tano wa Kenya.

“Wakati tunakuja kwa masuala ya Handshake, katika Kiswahili wanasema haya ni mambo ya ukora. Binafsi mimi siamini kabisa katika mambo hayo. Kusingekuwa na ile handshake, Raila angekuwa rais wa Kenya sasa hivi,” Owino alisisitiza vikali.

Owino alisema kuwa wao kama Azimio na haswa chama cha ODM ambacho ndicho kina ufuasi mkubwa katika muungano huo wameridhika kuwa wako upinzani na wataendelea kuikosoa serikali ya Ruto.

Alisema kuwa kitendo cha Odinga kuwarai viongozi wa Nyanza kumkaribisha Ruto eneo la Nyanza hakimaanishi kuwa anataka handshake bali ni kutokana na kuwa huyo ndiye kiongozi wa taifa sasa hivi na kwenda Nyanza kuzindua miradi ya maendeleo ni haki ya wakaazi wa eneo hilo kwani pia wao wanashiriki katika kulipa ushuru kwa njia ya utiifu mkubwa.

“Wazo la viongozi kuja pamoja ni nzuri kwa sababu lazima kuwe na Amani ili kuwe na maendeleo. Tunasema masuala ya kisiasa ndio yanatoa mwongozo katika masuala ya maendeleo ya nchi. Lakini kama hawatofanya maendeleo lazima tuwarekebishe,” Owino alisema.