Msemaji wa muungano wa upinzani Azimio la Umoja One Kenya msomi Makau Mutua amekashfu vikali mpango wa mkopo wa Hustler Fund uliozinduliwa na rais William Ruto mwaka jana.
Akizungumza katika mahojiano kwenye kituo kimoja cha runinga huku nchini, Mutua alisema kuwa kiwango kinachotolewa cha chini kabisa kwa mpango huo ni kidogo mno ambapo alikejeli kuwa hakiwezi hata kikamudu mtu kupata huduma nzuri za kinyozi.
"Hustler Fund ni mchezo, Wanaonufaika na Hustler Fund hawawezi hata kunyolewa nywele kwa Shilingi 500," Prof Mutua alisema kwenye mahojiano.
Mwaka jana baada ya uongozi wa Kenya Kwanza kuzindua rasmi mkopo huo, viongozi mbalimbali kutoka mrengo wa upinzani walitoa utabiri wao wakisema kuwa mpango huo haungefaulu hata kidogo.
Wengine waliwarai Wakenya kuchukua mkopo huo na kukaidi kulipa katika kile ambacho walisema ni pesa za serikali zilizokosa mpangilio maalum.
Lakini katika hotuba yake ya Jamhuri, rais Ruto aliwashangaza wengi alipotoa takwimu kuwa wengi wa Wakenya walionufaika kutoka kwa mkopo huo wamesharejesha pesa hizo huku wengine wakirudia kukopa tena.
Ruto alitoa ahadi kuwa sasa kiwango cha shilingi 500 ambacho mtu hupokea na baada ya kurudisha basi kiwango hicho kitaongozeka hadi shilingi 1000.
Aidha, rais Ruto alifichua kuwa baadhi ya viongozi wa upinzani waliokuwa wakiwataka wananchi kutorudisha pesa hizo wao wanakopa kinyemela na kurudisha huku wakijaribu kuwapotisha wananchi wa chini.
Mutua alikosoa serikali pia kwa hatua ya kuanza kuweka tozo kwa miamala ya M-Pesa.