Mzee mmoja katika kaunti ya Kisii analilia haki baada ya watoto wake wa kambo kumgeuka na sasa wanataka kumfukuza kutoka kwa boma lake.
Kulingana na video ambayo ilipakiwa na blogu moja kutoka kaunti hiyo isiyokosa vituko, mzee huyo kwa jina Machuka alimuoa mwanamke miaka kadhaa iliyopita akiwa na watoto wa kiume wawili.
Kwa bahati alifanikiwa kuzaa na mwanamke huyo watoto wengine wa kike pekee, ambao sasa hawako nyumbani na amebaki na wa kiume ambao walikuja na mama yao.
Aliwahangaikia wavulana hao mpaka sasa wamekuwa watu wazima ambapo wamemgeuka katika kile blogu hiyo iliripoti kuwa hawataki kumsikia akishiriki mapenzi na mama yao.
Mzee huyo ambaye sasa alifika mbele ya mahakama ya kaunti hiyo kutoa malalamishi yake alieleza kwamba watoto hao huwa wanasubiri wakati ameingia chumbani na mke wake ambaye ni mama yao, wanawafumania kwa fujo, kumtia mijeledi kabla ya kumuhamisha mama yao kutoka chumba hicho kwenda chumba kingine.
Imefikia hatua sasa mzee huyo amefukuzwa katika boma lake na watoto wake wa kambo ambapo amelazimika kukodisha nyumba mbali kwa kuogopa kurudi nyumbani tena, huku pia akisema mali yake imeharibiwa na vijana hao ambao wengine wako na kazi za maana kwenye jamii.
Mzee huyo alisema kuwa amejaribu mara kadhaa kuripoti visa hivyo kwa polisi lakini kwa kuwa vijana hao wake wana pesa, huwa wanawatumia pesa na kumgeukia mzee huyo kabla ya kumtia ndani.
“Mimi nalia, nakimbizwa na watoto nilioa mama yao akiwa nao. Niliwaleta kwangu nikafanya kazi kuwasomesha, lakini sasa wamenifukuza nyumbani nikaenda kukodisha nyumba huko mbali kuishi. Walinifuata hadi kanisani wakitaka kunipiga. Hawa watoto niliwaleta kama watoto wangu, sasa wananiona kama nyang’au wanataka kuniua,” mzee huyo alisema.
Mzee huyo sasa alikuwa analilia haki kutoka kwa vyombo vya dola kumsaidia ili apate Amani yake kama mkenya dhidi ya kuhangaishwa na vijana hao wake.
Mzee huyo alisema alimuoa mwanamke huyo na watoto wa kiume wawili na akazaa naye wasichana pekee wala hakupata wa kiume na yeye.
Kwa uchungu, alisema kijana yake mmoja alienda akamletea mama yao kitanda chake na kumhamishia huko kutoka kwa chumba cha mzee baba yao.