Kisii: Mwalimu ajitoa uhai baada ya kugundua ana saratani ya kibofu

Mwalimu huyo aliacha barua akielezea kuwa tangu mwaka 2015 amekuwa akikumbwa na matatizo ya afya, la hivi karibuni likiwa saratani.

Muhtasari

• Katika barua yake, alimtaka mkewe kuendelea kumtunza mama yake na kuwalea watoto wao.

• Mwalimu huyo alikuwa anafunza masomo ya kemia na hisabati.

Mwalimu mmoja wa shule ya upili kaunti ya Kisii ajiua kwa kujitoa uhai baada ya kugundua kuwa anaugua saratani.

Mwalimu huyo kwa jina Evans Onchari mwenye umri wa miaka 45 alikuwa anafunza masomo ya kemia na hisabati katika shule ya upili ya Senior Chief Musa Nyandusi Kegati, eneobunge la Nyaribari Chache kaunti ya Kisii.

Mwalimu huyo anaarifiwa kujiua usiku wa Jumapili na kuacha barua yenye maelezo ya sababu ya kuchukua uamuzi huo huku akiorodhesa sababu nne kuu za kujiua.

Katika barua aliyoiacha, Onchari alisema tangu mwaka wa 2015 hali yake ya afya haijakuwa sawa kwani ndio mwaka aligundua ana ugonjwa wa pumu, kisha mwaka 2021 tena akaambiwa na madaktari kuwa anaugua ugonjwa wa presha na mapema mwaka huu amegundua anaugua saratani ya kibofu.

"Pumu sugu mnamo 2015, shinikizo la damu mnamo 2021, saratani ya kibofu mnamo 2023 na iliashiria kuvimba kwa muda mrefu mnamo 2023," aliandika.

Mwalimu Onchari alimtakia mke wake kila la kheri katika maisha yake kama mjane huku akimtaka kuendelea kuwalea na kuwatunza watoto wao na mama yake kama ambavyo amekuwa akimtunza katika miaka 7 ya matatizo yake ya afya.

“Asante mke wangu kwa kunitunza katika miaka saba iliyopita katika hali yangu. Mtunze mama Sabina na watoto wetu wote,” mwalimu alimalizia maelezo yake kisha akaweka sahihi yake mwishoni.