Sonko ajitokeza kumpeleka shule msichana aliyemlilia kwa msaada wa karo

Msichana huyo alisema mama yake ni singo na hana kazi kando na kumlea pia nyanya yao.

Muhtasari

• “Mama ameshalipa elfu 11 na salio ni elfu 17, pia sare na malazi ni elfu 34 naomba unisaidie" - msichana huyo aliomba.

Msichana aliyetoa ombi kwa Sonko
Msichana aliyetoa ombi kwa Sonko
Image: Screengrab

Hatimaye mfanyibiashara Mike Sonko amejitoa kumsaidia mwanafunzi mmoja ambaye video yake ilisambaa akimtumia Sonko ujumbe wa kutaka msaada ili kujiunga na shule ya upili.

Katika video hiyo, msichana huyo kwa jina Margret Koki kutoka Ikalakala Matuu anasema aliitwa katika shule ya upili ya wasichana ya State House na alifaa kujiunga siku ya mwisho kabisa Jumatatu lakini hilo halikuwezekana kutokana na uhaba wa karo.

“Mimi ni Margret Koki kutoka Matuu, niliitwac shule ya wasichana ya State House na nilifaa kujiunga JUmatatu siku ya mwisho lakini haikuwezekana. Mama yangu ni singo na hana kazi na pia anamlea bibi yangu…” msichana huyo alisema katika ujumbe wake kwa Sonko.

Aliendelea kuratibu vitu ambavyo alitakikana kuwa navyo ili kujiunga na shule hiyo ila akasema mama yake angalau amefanikiwa kulipa karo shilingi elfu 11 na salio la elfu 17 limemfanya kutojiunga na shule hiyo huku akimtaka Sonko kumpa msaada.

“Mama ameshalipa elfu 11 na salio ni elfu 17, pia sare na malazi ni elfu 34 naomba unisaidie kwa sababu  pia nataka kusoma ili nije kuwasaida maskini baada ya masomo yangu ili pia wajinufaishe kielimu,” msichana huyo alisema.

Sonko aliona video hiyo na kutoa nambari yake ya mawasiliano akiwataka yeyote mwenye uwezo wa kuifikia familia yake kumpigia simu mwisho kabisa Jumanne jioni.

“Nimekutana na video hii kwenye mitandao ya kijamii, je wazazi wa binti huyu mkali ambaye ameitwa Statehouse Girls kufika ofisini kwangu mara moja na sio baada ya leo, wanitafute. Binti huyu lazima aende shule leo, tunapaswa kuunga mkono kizazi kijacho ambao ni viongozi wa kesho,” Sonko alisema.