"Tutapotea Nairobi!" - KOT wasema jumba la OTC likivuliwa neti ya kijani ya muda mrefu

Wakenya Twitter walisambaza picha ya jumba hilo likivuliwa neti ya kijani na kupewa muonekano mpya. Limekuwa na neti hiyo kwa karibu miaka 10.

Muhtasari

• Jumba la OTC limekuwa ndani ya neti ya kijani kwa karibu miaka 10 hadi kugeuzwa kirejeleo cha maelezo ya alipo mtu jijini.

• Sasa wengi waliokuwa wakilitegemea kutoa maelezo hayo watalazimika kutafuta kitu kingine cha kipekee.

Jumba la OTC lapata muonekano mpya
Jumba la OTC lapata muonekano mpya
Image: Twitter

Mahsabiki na watumizi wa mtandao wa Twitter jijini Nairobi wamefurika kutoa maoni yao kuhusu kumalizika kwa jumba lililopo katikati mwa jiji eneo la OTC ambalo limekuwa chini ya ujenzi kwa miaka Zaidi ya 1o.

Jumba hilo kwa mara nyingine tena limekuwa gumzo kubwa kwenye mtandao wa Twitter, picha zikienezwa ambazo zinaonesha hatua za mwisho kabisa zikiendelea, zikiwemo ni pamoja na kuondolewa kwa neti ya kijani ambayo imekuwa ikilifunika kwa muda huo wote tangu ujenzi wake ulipoanza.

Watumizi wa Twitter walizua utani kuwa pindi jumba hilo litakapozinduliwa tayari kwa matumizi ya biashara za umma, huo utakuwa ni mwanzo wa watu haswa wageni wanaotembelea jiji kuu la Kenya kupotea.

Kulingana na walioneza dhana hii, jumba hilo kwa miaka hiyo yote limekuwa likitumiwa kama kigezo cha kutoa maelezo ya alipo mtu jijini Nairobi kwa kurejelea kwamba ako karibu na jumba hilo lililopo katika soko la OTC.

Lakini sasa wengi huenda watapoteleana kwa sababu “lile jumba la neti ya kijani” halitakuwepo tena, kwani litakuwa kama jumba lolote la kibiashara lisilo la ishara ya kipekee kulitofautisha na majumba mengine ya kibiashara yaliyopo OTC.

“Neti ya kijani kwenye jengo maarufu la OTC ikiondolewa wakati ujenzi unakaribia kukamilika. Ni wakati sasa wa watu kuanza kupotea Nairobi,” mmoja aliasema.

Wengine walisema kwamba mwenye jumba hilo amewataka Wakenya kupendekeza jina la kipekee litakalopewa jumba hilo huku wengine pia wakivuta duka la jumla la China Square na kulitaka kuchukua hatua za haraka kukodisha jumba hilo ili kufungua biashara yao ya bidhaa za bei nafuu kule.

“China Square inapaswa kukodisha jengo hilo la OTC kwanza kabisa na kuua wauzaji wanaodaiwa kuwa katikati ya jiji,” Marley Juan alipendekeza.

“Mmiliki wa jengo la OTC anawaomba Wakenya kupendekeza jina la jengo hilo. Hivi karibuni watu watapotea,” Elias Chirchir alisema.

Ripoti ya awali inaonesha kwamba jumba hilo lilifunikwa kwa neti ya kijani takribani miaka 15 iliyopita baada ya kununuliwa na mfanyibiashara mmoja.

Hata hivyo, ujenzi wa kulikarabati ulikumbwa na msukosuko kutokana na mmiliki huyo mpya na mmoja wa wafanyibiashara waliokuwa wamelikodisha ambao hawakuwa wanataka kuhamishwa ili kupisha ukarabati, kwa kile kilitajwa kuwa kodi yao haikuwa imekamilika.

Zogo hilo liliishia mahakamani kufanya ukarabati kusitishwa kwa miaka mingi hadi kulifanya jumba hilo kuwa kama kirejeleo cha kutoa maelezo ya alipo mtu jijini.