Mwili wa mwanamke aliyetoweka wapatikana umezikwa katika boma la jirani yake

Jamaa mweney boma alisafiri kutoka Kitengela kwenda nyumbani kujenga nyumba, wakati anachimba mchanga, akakumbana na mabaki ya maiti.

Muhtasari

• Familia ya mwanamke huyo ilisema walipiga ripoti kuhusu kupotea kwake, watuhumiwa wakashikwa lakini baadae kuachiliwa huru.

• Mwili huo ulifukuliwa kikamilifu na kupelekwa katika hospitali ya Kakamega kwa uchunguzi wa kina.

Polisi katika kaunti ya Kakamega wanachunguza kisa cha ajabu ambapo mwanamke aliyeripotiwa kutoweka miezi michache iliyopita kupatikana amezikwa katika boma la jirani yake.

Kulingana na taarifa moja runingani Citizen, kisa hicho kiliripotiwa kutokea katika eneobunge la Ikolomani kaunti ya Kakamega ambapo mwili huo ulipatikana na mwanamume mmoja aliyekuwa akichimba udongo kwa ajili ya matumizi kwa nyumba yake mpya kabla ya kuupata mwili huo.

Fabian Muteshi, mkaazi wa Kitengela alisafiri kwenda nyumbani kwao Ikolomani kwa ajili ya ujenzi wa nyumba yake, katika harakati za kuchimba mchanga, alifikia mabaki ya mwili wa mtu ambayo yalidhaniwa kuwa ya mwanamke huyo aliyeripotiwa kutoweka.

"Nilikuwa nikivuna udongo wa udongo kwa ajili ya nyumba yangu mpya ninayojenga, ndipo nilipokuta fuvu la kichwa cha binadamu likiwa na viungo vingine vya mwili. Sijawahi kuogopa hivyo," Muteshi aliiambia Citizen.

Familia moja ilijitokeza na kuutambua mwili huo kuwa wa mpendwa wao Rosa Kamoya, mwenye umri wa miaka 37 aliyeripotiwa kutoweka nyumbani kwa njia za utata mwezi Septemba mwaka jana.

Baba yake marehemu huyo alisema kwamba bintiye alitoweka mwaka jana akiwa na dada zake wawili katika kijiji jirani na tangu siku hiyo juhudi za kumtafuta zimeambulia patupu kwa Zaidi ya miezi 7 sasa.

Mwili huo ulifukuliwa kutoka hapo na kupelekwa katik hospitali ya Kakamega ukisubiri uchunguzi Zaidi wa maiti.