Wakenya 3.1M hutumia pombe, Mt Kenya inaongozwa kwa unywaji wa pombe kali

Wakati Mlima Kenya wanaongoza kwa unywaji wa pombe kali, eneo la Magharibi linaongoza kwa matumizi ya pombe kwa jumla.

Muhtasari

• Ripoti hiyo ilisema kwamba eneo la Magharibi inaongoza kwa matumizi ya vileo likifuatwa na Pwani, Mlima Kenya na kisha Nairobi.

• Hata hivyo, Mlima Kenya wanaongoza kwa matumizi ya pombe kali wakifuatwa na Pwani, Bonde la Ufa kisha Nairobi.

pOMBE KALI HUNYIWA SANA MT KENYA
pOMBE KALI HUNYIWA SANA MT KENYA
Image: NACADA

Janga la ulevi ni sugu na ambalo limekuwa likikita mizizi yake katika eneo pana la Mlima Kenya kwa miongo kadhaa sasa huku juhudi za kulitokomeza zikionekana kubuma aghalabu.

Ni miezi minne tu baada ya rais William Ruto kuagiza maafisa wa usalama kukabiliana na pombe haramu katika eneo hilo lakini ufichuzi mpya uliofanywa na runinga ya Citizen unaonesha kwamba suala la pombe haramu bado ni sugu katika eneo hilo.

Pombe haramu bado inatishia maisha ya vijana wengi na kulemaza ubora wao katika jamii.

Halimashauri ya kukabiliana na utumizi wa pombe NACADA inasema kwamba pombe takriban lita milioni moja imenaswa na kumwagwa katika muda wa miezi miwili iliyopita.

Katika Makala hayo yaliyopeperushwa kwa jina la ‘Kinanda cha ulevi’ waathirika mbalimbali wa ulevi walionekana wakiwa katika hali ya kutamausha na kutia huruma, wakijikongoja kwa kuyumba kutokana na ulevi.

Wengine walionekana wakiwa walevi majira ya asubuhi sana, mpaka mtu unashangaa ni sehemu gani hiyo ya kuuza mvinyo ambayo inafungua milango yake asubuhi kipindi ambacho wengi wanatarajiwa kuhangaika na riziki.

“Kuna chang’aa ya kuchemshwa na kuna ile nyingine, kikombe moja wananunua 500 na inatengeneza pombe mtungi moja na atauza elfu 6. Ni ile ya kemikali yenye inafanya watu wanapoteza macho unakuwa kipofu,” mtu mmoja asiyetaka kujulikana alisema.

Mbunge wa Gatundu North, Elijah Njoroge alisema ili pombe kufutwa kabisa katika eneo hilo, kunahitaji ushirikiano wa washikadau wote ikianza na familia na jamii.

“Serikali haiwezi maliza pombe haramu bila kushirikiana na wanakijiji wa hicho kijiji. Ukishika mtoto wa mtu, kesho anakuja kumtoa jela na atarudi tu katika kuipika na kuitumia,” mbunge huyo alisema.

Kulingana na ripoti ya NACADA, wakenya milioni 4.7 hutumia vileo na dawa za kulevya huku milioni 3.1 wakiwa ni watumizi wa pombe pekee.

Ripoti hiyo ilisema kwamba eneo la Magharibi inaongoza kwa matumizi ya vileo likifuatwa na Pwani, Mlima Kenya na kisha Nairobi.

Hata hivyo, Mlima Kenya wanaongoza kwa matumizi ya pombe kali wakifuatwa na Pwani, Bonde la Ufa kisha Nairobi.