Winnie Odinga azungumzia kuhusu kufanya kazi na Charlene Ruto

Winnie na Charlene ambaye ni bintiye Rais William Ruto, mnamo Ijumaa, Machi 10, walishiriki jukwaa la kutetea Haki za Wanawake

Muhtasari
  • Aidha, akitoa maoni yake kuhusu mfumo wa uchaguzi nchini, Winnie alisema kuwa uchaguzi umekuwa wa kawaida tu
WINNIE ODINGA
Image: KWA HISANI

Winnie Odinga mnamo Jumatatu, Machi 13, alisema kuwa kufanya kazi na Charlene Ruto haikuwa changamoto kwake akisema kuwa mamlaka ya kisiasa haikuwa lengo lake.

Akizungumza na chombo cha habari cha Afrika Kusini News 24, bintiye Raila Odinga alieleza kuwa wao ni kizazi kipya cha Waafrika na ilikuwa muhimu kwao kufanya kazi pamoja ili kuboresha maisha ya wengine.

Winnie na Charlene ambaye ni bintiye Rais William Ruto, mnamo Ijumaa, Machi 10, walishiriki jukwaa la kutetea Haki za Wanawake katika Kongamano la 22 la Kenya Model United Nations, ambapo walishughulikia masuala mbalimbali yanayoathiri wanawake katika vizazi tofauti.

"Sioni kama changamoto kwa sababu lazima isiwe moja. Tunapaswa kubadili fikra zetu kama Waafrika. Nguvu ya kisiasa sio lengo.

“Sisi ambao tumebahatika kuwa na baba tunahitaji kufanya kazi pamoja ili kuwapa ndugu na dada zetu maisha yenye heshima. Hilo ndilo lengo,” Winnie alisema.

Aidha, akitoa maoni yake kuhusu mfumo wa uchaguzi nchini, Winnie alisema kuwa uchaguzi umekuwa wa kawaida tu.

Aliongeza kuwa matakwa ya wananchi yalikandamizwa wakati wa uchaguzi na mshindi aliamuliwa na wengine.

"Tumeshindwa kizazi kilichopita ambacho kilifanya kazi kwa bidii ili mataifa yetu yawe huru. Inaonekana kuna mlango wa ukoloni mamboleo kupitia kura.

"Ninaamini kuwa ni wakati wa kuzaliwa kwa sheria ya kisiasa iliyofikiriwa upya barani Afrika. Moja ambayo inakubali tofauti zetu za kitamaduni, inakubali tofauti na inafanya kazi kwa watu. Hatuendi popote,” aliongeza Winnie.