Mama wa taifa Rachel Ruto amkumbatia kijana mdogo, amruhusu kuketi mapajani mwake

"Wewe ni mama halisi Mungu akubariki sana hata unapotenda mema" mmoja alimhongera.

Muhtasari

• Rachel aliungana na viongozi wa kaunti ya Nairobi kugawa chakula cha msaada Korogocho.

Maam Rachel Ruto amkumbatia kijana mdogo Korogocho.
Maam Rachel Ruto amkumbatia kijana mdogo Korogocho.
Image: Twitter

Mama wa taifa Rachel Ruto amefurahisha amefurahisha wengi na kupokezwa sifa kede kede mitandaoni baada ya kuonekana amempakata kijana mdogo aliyepanda jukwaani alikokuwac ameketi pamoja na viongozi wengine.

Katika picha ambazo alipakia kwenye ukurasa wake wa Twitter, mama wa taifa alikuwa amejumuika na viongozi wengine wa kaunti ya Nairobi wakiongozwa na gavana Sakaja katka ugavi wa chakula cha msaada katika mitaa duni ya Nairobi.

Safari hii ilikuwa ni ya wakaazi wa mtaa duni wa Korogocho kupokezwa ahadi ya chakula cha msaada waliyopewac wiki jana na Rachel alipokuwa jukwaani, kijana mmoja mdogo alimvizia na kumkumbatia kwa upendo mkubwa.

Kijana huyo alikuwa amevalia surupwenye la rangi ya manjano na mama wa taifa anaonekana akimkumbatia kabla ya kumuinua juu na kumketisha kwenye mapaja yake akitabasamu kwa furaha.

Katika hafla hiyo ya kugawa chakula cha msaada, mama Rachel alisema kwamba haiwezekani nchi kuendelea bila watu kutoa msaada kwa walio na matatizo.

“Ni muhimu tuchukue hatua za pamoja na shirikishi ili kukabiliana na janga la chakula ambalo limeletwa na athari za mabadiliko ya hali ya hewa. Juhudi zetu za pamoja kama taifa lazima zielekezwe katika kusaidia na kuwawezesha walio hatarini zaidi miongoni mwetu,” mama wa taifa alisema.

“Kwa kuunganisha rasilimali zetu na nguvu zetu, tunaweza kuunda nguvu kubwa ya kufanya mema katika jamii zetu, haswa wakati wa shida kama vile njaa ya sasa.”