Sudi atema moto wa vitisho kwa wafanyikazi wa serikali watakaokosa kufika kazini Jumatatu

"Na nimesikia eti Jumatatu ni likizo, wacha tupate mfanyikazi yeyote wa serikali hajafika kazini, ndio mtajua, na tunawangoja sana" - Sudi alisema.

Muhtasari

• "Na wacha kuchukuliwa kama Wajinga. Kwani hawa watu wenu wanaibiwa kila siku kwani wao hawajui wanachokifanya?” Sudi.

Ooscar Sudi atishia watakaochukua likizo ya maandamano
Ooscar Sudi atishia watakaochukua likizo ya maandamano
Image: Maktaba

Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi ametema moto wa cheche za vitisho kwa wafanyikazi wa serikali kote nchini ambao wanapanga kuchukua likizo ya mapumziko Jumatatu ya Machi 20.

Muungano wa upinzani ukiongozwa na Raila Odinga unatarajiwa kuongoza maandamano makubwa nchini kote kuanzia Jumatatu na Odinga aliwataka Wakenya kuchukua sku hiyo kama likizo ya kitaifa kwa ajili ya mapumziko kazini na kujiunga naye katika maandamano.

Azimio wanasema kwamba maandamano yao yanalenga kutoa lalama zao kwa kile wanasema ni kuibiwa Kura za Agosti mwaka jana na pia kupanda kwa gharama ya maisha tangu Ruto achukue hatamu kama rais wa tano.

Kufuatia agizo hilo la Odinga kutaka Wakenya wachukue Jumatatu kama likizo, mbunge huyo mwandani wa Ruto ametoa onyo akisema kwamba watachukuliwa hatua kali, haswa wale ambao wanafanya kazi za serikali.

“Na nimesikia eti Jumatatu sijui ni likizo, wacha tupate mtu yeyote hajaenda kazi ya serikali, ndio mtajua. Na tunawangoja sana. Na wacha kuchukuliwa kama Wajinga. Kwani hawa watu wenu wanaibiwa kila siku kwani wao hawajui wanachokifanya?” Sudi alisema kwa sauti ya vitisho.

Sudi alisema kwamba hali ngumu ya maisha nchini ilianza kuwa ngumu kipindi Odinga alifanya maridhiano ya Amani na rais mstaafu Uhuru Kenyatta, akisema kwamba kipindi hicho Odinga alikuwa amenyamaza.

“Wakati uchumi ulikuwa unaenda chini, wewe Baba ulikuwa umenyamaza tu unaona tu nchi ikienda hivi, wacha turekebishe nchi yetu irudi penye inafaa. Na msituletee. Hakuna mke wa mtu au hakuna mtu ako na mimba ya mtu hapa mjini…” Sudi alisema.