CS Nawamba asifiwa mitandaoni kwa kukubali kumzika aliyekuwa mke wake katika boma lake

Ababu Namwamba walitengana na mama wa watoto wake watatu takriban miaka 4 iliyopita.

Muhtasari

• Misa ya wafu ya Priscah Mwaro ilifanyika Ijumaa katika kanisa la Consolata Shrines jijini Nairobi.

• Ababu aliongozana na wanawe watatu katika kuhudhuria misa hiyo.

• Mwaro anatarajiwa kuzikwa Jumamosi katika boma la Namwamba kaunti ya Busia.

Ababu Namwamba na wanawe katika misa ya wafu ya aliyekuwa mke wake.
Ababu Namwamba na wanawe katika misa ya wafu ya aliyekuwa mke wake.
Image: Hisani

Aliyekuwa mke wa waziri wa michezo na vijana Ababu Namwamba, Priscah Mwaro atazikwa Jumamosi katika boma la mbunge huyo wa zamani wa Budalangi, kaunti ya Busia.

Waziri wa Michezo Ababu Namwamba mnamo Ijumaa alihudhuria misa ya wafu ya aliyekuwa mke wake Priscah Mwaro.

Misa hiyo ilifanyika katika Kanisa la Consolata Shrine huko Westlands, Nairobi. Mwaro alipatikana amekufa nyumbani kwake Nairobi mnamo Machi 8.

Aliolewa na Namwamba kwa miaka minane, na kwa pamoja walikuwa na watoto watatu. Waliachana mnamo 2019.

Katika misa hiyo ya wafu Ijumaa, Namwamba aliongozana na watoto wake watatu pamoja na watu wa karibu kumpa heshima za mwisho aliyekuwa mke wake.

Marehemu alikuwa amesherehekea siku yake ya kuzaliwa mnamo Jumanne, Machi 7, saa chache kabla ya kifo chake cha ghafla.

Mwaro akitokea Kaunti ya Busia, alihitimu mwaka wa 2015 na Shahada ya Kwanza ya Biashara (Rasilimali Watu) kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi.

Awali wakati wa kifo chake, wengi walidhani kwamba Namwamba angejitenga na kifo hicho ikizingatiwa kwamba walishatengana Zaidi ya miaka minne iliyopita lakini kwa roho ya kiume, waziri huyo alikubali kuwa angempa heshima za mwisho Mwaro kwani ni mama wa watoto wake watatu, ambao Namwamba alikuwa akiishi nao baada ya mama yao kuondoka.

Watu walimsifia Namwamba mitandaoni wakimtaja kama mwanamume mwenye roho ya kusamehe na kusahau yaliyopita.