DP Gachagua arudi kileleni mwa Mlima Kenya kutoa shukrani kwa Mungu kushusha mvua

Gachagua alisema kabla ya maombi yao, ukame mkali ulioshuhudiwa nchini haukuwa umeshuhudiwa kwa miaka 40 iliyopita!

Muhtasari

• Kando na shukrani za mvua, DP pia aliombea mvua zaidi na mavuno mengi kwa taifa la Kenya msimu wa upanzi unapiong'oa nanga.

Gachagua arudi mlimani Kenya kushukuru Mungu kwa mvua.
Gachagua arudi mlimani Kenya kushukuru Mungu kwa mvua.
Image: Twitter

Naibu wa rais Rigathi Gachagua kwa mara nyingine tena amefanya ziara ya Mlima Kenya.

Safari hii, hajaenda kuomba kitu chochote bali ni ziara ya kutoa shukrani kwa Mungu kwa kujibu maombi ya kuleta mvua.

Itakumbukwa miezi michache nyuma, Gachagua alionekana mlima Kenya akifanya ziara ambayo aliitaja kama ni ya kuomba Mungu kushusha mvua ili kukata kiangazi kilichokuwa kimmeramba sehemu nyingi za nchi.

Pia katika ziara hiyo, Gachagua alimshukuru Mungu kwa kuwapa ushindi yeye na rais William Ruto.

Ila baada ya mvua kunyesha kwa wiki mapema wiki hii, Gachagua kwa mara nyingine tena amerudi mlimani kumshukuru Mungu kwa kujibu maombi yao ambayo walikongamana katika uga wa Nyayo mwezi Februari kwa ajili ya kuombea mvua.

Gachagua alisema kwamba kabla ya kufanya maombi, ukame mkali ulikuwa umemeza maeneo mengi nchini, ambao aliutaja kuwa ukame mbaya na ambao haukuwahi shuhudiwa nchini kwa Zaidi ya miaka 40 iliyopita.

“Asubuhi na mapema, nilirudi Mlimani kumshukuru Mungu kwa mvua. Nilichukua muda kumshukuru Mwenyezi kwa Neema na Rehema zake kwa kutupa mvua baada ya kushindwa kwa misimu mitano mfululizo - ukame mbaya zaidi katika miaka 40,” Gachagua alisema kupitia msururu wa picha alizozipakia kwenye ukurasa wake wa Twitter.

 Baada ya kutoa shukrani kwa mvua, mlokole naibu rais pia alitoa ombi moja la mwisho kwa Mungu;

“Nilimwomba Mungu, kutoka chini ya Mlima Kenya, atupe mvua zaidi na mavuno mengi.”