Mshauri wa Raila, Jakakimba ajiuzulu ODM siku chache baada ya Winnie Odinga kumtusi

Kujiuzulu kwake kama mwanachama kunakuja siku mbili tu kuelekea maandamano makubwa ya Jumatatu yatakayoongozwa na Odinga.

Muhtasari

• Licha ya kuonekana kutofautiana vikali na binti wa Odinga, Jakakimba alimsifia pakubwa Odinga kwa kumkuza na kumlea kisiasa tangu 2004.

• Jakakimba amekuwa mshauri wa karibu wa kisiasa wa Raila Odinga na kwa wakati mmoja aliwahi kuwa kama msaidizi wake wa kibinafsi.

Silas Jakakimba
Silas Jakakimba
Image: Instagram KWA HISANI

Mwanasiasa Silas Jakakimba, mshirika wa Raila Odinga, amejiuzulu kama mwanachama wa maisha wa chama cha ODM, siku mbili tu kuelekea maandamano ya Jumatatu dhidi ya serikali ya William Ruto.

Jakakimba ambaye kwa muda mrefu amekuwa akihudumu kama msaidizi wa karibu wa Odinga aliandikia msajili wav vyama vya kisiasa barua ya kutaka kuondolewa kutoka sajili ya wanachama wa ODM, mara moja.

"Naomba utimize uamuzi huu kwa kufuta jina langu kwenye daftari rasmi la wanachama wa ODM," sehemu ya barua yake kwa ORPP ilisema.

Katika barua hiyo yenye maelezo marefu na ambayo yalikuwa yanamsifia na kumvisha koja la maujai ghali bwana Odinga, Jakakimba alifichua kwamba mara ya kwanza walikutana na Odinga mwaka 2004 na mpaka sasa amemlea na kumkuza pakubwa katika fani nyingi za maisha.

"Kwa shukrani na heshima nyingi, Jakom, pokea uhakikisho wa heshima yangu ya juu, kuzingatia na maombi kwa ajili ya afya yako nzuri na maisha marefu ya furaha. Nimebahatika kushiriki katika fahari adimu ambayo nimekuwa pamoja nanyi huku mkipeana changamoto kadhaa kuona marekebisho ya usanifu wa utawala wetu wa wakati huo na kuwa utawala wa katiba mpya ulioratibu ugatuzi katika kitovu cha utawala wetu," alisema.

Hadi kujiuzulu kwake, mwanasiasa huyo alikuwa akihudumu kama mshauri wa Bw Odinga. Mnamo 2007, alihudumu kiongozi wa ODM kama msaidizi wake wa kibinafsi bungeni.

Kujiuzulu kwake kunakuja siku chache tu baada ya kupapurana mitandaoni na binti wa Raila Odinga, Winnie Odinga.

Jakakimba alilalamika vikali kwenye ukurasa wake wa Twitter jinsi Winnie alimtumia neno la matusi kwa kile alisema kwamba ni kutokana na uamuzi wake wa kutumia picha ya pamoja akisalimiana na rais Ruto kwenye jalada lake Twitter.