Nakuru: Wanaume 2 wavua nguo zote na kukwea mti nje ya polisi kabla ya kuanza kuhubiri

Wawili hao walifika mwendo wa 6AM na kukwea mti huo na polisi walijaribu kuwashawishi kushuk wakadinda, mwendo wa 12:30PM ndio walibembelezwa na kushuka.

Muhtasari

• Maafisa wa polisi waliwaweka wawili hao kizuizini ili kujaribu kupata maelezo kutoka kwao.

• Klipu inayoonesha wawili hao wakiwa uchi shughulini juu ya mti ilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Wahubiri uchi mtini jijini Nakuru.
Wahubiri uchi mtini jijini Nakuru.
Image: Sxcreengrab// YouTube

Kisa cha ajabu kilishuhudiwa mjini Nakuru baada ya wanaume wawili kudaiwa kufika mjini hapo karibu na kituo cha polisi kisha kupanda juu ya mti na kuvua nguo zote kabla ya kuanza kuhubiri kwa sauti.

"Wanaume hao wawili walifika eneo la tukio na kuvua nguo kabla ya kupanda juu ya mti na kuanza kuhubiri. Haijabainika ni kwa nini waliamua kusababisha kisanga nje ya kituo cha polisi," mmoja aliyeshuhudia kisa hicho alisema.

Haijabainika ni kwa nini wawili hao walichagua mtu ulioko nje ya kituo cha polisi cha kati jijini Nakuru.

Wakaazi walisema wawili hao walijaribu kuchukua hatua hiyo ya kipekee Alhamisi usiku lakini wakafukuzwa na maafisa wa polisi waliokuwa wakisimamia kituo hicho, jambo ambalo lilizua taharuki.

Mapema Ijumaa, walioshuhudia walisema walifika eneo hilo mwendo wa saa kumi na mbili asubuhi, wakavua nguo na kupanda juu ya mti bila ya maafisa wa polisi kujua.

Kipande cha video cha kitendo chao, ambacho kimezua mjadala kwenye mitandao ya kijamii, kinawaonyesha wakihubiri na kunukuu mistari ya Biblia, bila wasiwasi. Umati unakusanyika haraka ili kutazama drama inayoendelea.

Maafisa wa polisi waliwaweka wawili hao kizuizini ili kujaribu kupata maelezo kutoka kwao.

Bw Masika, kamanda wa polisi eneo la Nakuru Mashariki alisema juhudi zao za kuwashawishi kuvalia na kushuka kutoka kwenye mti huo hazikufaulu, lakini hatimaye wananchi waliwashawishi kufanya hivyo mwendo wa saa 12:30 mchana.