Msichana wa miaka 16 amuua mamake kwa kumnyima uhuru wake na 'kumkazia maisha'

Msichana huyo alishirikiana na mshikaji wake na walimsubiri mamake usiku kabla ya kumpiga kwa kikaango na kuburura mwili wake hadi kitandani mwake.

Muhtasari

• "Msichana ... alikuwa na mazungumzo ambayo aliripotiwa kumwambia kuwa mama yake, 44, alikuwa akimnyima uhuru wake" taarifa ya polisi ilisoma.

• Kijana huyo alikamatwa na kushtakiwa kwa mauaji huku msako wa kumtafuta mwendazake ukianzishwa.

Polisi
Image: Maktaba

Msichana wa miaka 16 amewekwa chini ya ulinzi wa polisi kufuatia kushukiwa kumuua mama yake kwa kile vyombo vya dola vilitaja kuwa ni marehemu mama yake kumnyima uhuru wa kufanya mambo kivyake.

Kulingana na jarida la Times Live nchini Afrika Kusini, polisi katika ukanda wa Limpompo wanamshikilia msichana huyo na msako dhidi ya waliyeshirikiana naye kufanikisha kifo cha mama yake unaendelea.

Kisa hicho kilitokea Jumatano mwendo wa saa nne usiku katika bustani ya Lesedi.

Msemaji wa polisi wa Limpopo Brig Motlafela Mojapelo alisema msichana huyo anadaiwa kukutana na "mshikaji" wake karibu na nyumba yake viungani mwa Polokwane.

"Msichana ... alikuwa na mazungumzo ambayo aliripotiwa kumwambia kuwa mama yake, 44, alikuwa akimnyima uhuru wake na kwamba alitaka kuachana naye. Wawili hao kisha wakaenda nyumbani kumsubiri mamake msichana. Mama huyo alifika nyumbani na inaonekana alishambuliwa kwa kikaango na kuanguka. Inaripotiwa kuwa mshukiwa alizidi kumnyonga. Baada ya hapo wakamkokota hadi chumbani na kuondoka zao,” Jarida hilo iliripoti.

Msichana [wakati huo] alilala kwenye gari la mamake usiku huo na aliripoti kisa hicho kwa polisi siku iliyofuata Machi 16 na kudai kwamba alimpata mamake kwenye dimbwi la damu.

Kesi ya mauaji ilifunguliwa na wakati wa uchunguzi wa awali, ikabainika kuwa msichana huyo alidaiwa kupanga njama na mshukiwa kumuua mamake kwa sababu alitaka uhuru wake mwenyewe, Mojapelo alisema.

“Kijana huyo alikamatwa na kushtakiwa kwa mauaji huku msako wa kumtafuta mwendazake ukianzishwa. Msichana huyo mwenye umri wa miaka 16 alifikishwa katika mahakama ya Polokwane siku ya Ijumaa kwa shtaka la mauaji na kesi ilirejeshwa hadi Aprili 4 kwa uchunguzi zaidi wa polisi,” taarifa ilisema.

 

"Polisi wanaita 'Lebalang' kujitolea katika kituo cha polisi kilicho karibu ili kusaidia katika uchunguzi," aliongeza.