Huku zoezi la kufukua maiti ya waumini wa dhehebu potovu la pasta Mackenzie ukiendelea sambamba na shughuli ya kuwatafuta na kuwaokoa waumini wengine ambao wamejificha katika shamba la ekari 800 huko Shakahola, wiki jana polisi walimkatama mwanamume mmoja ambaye alitajwa kuwa ‘mtu wa mkono’ wa mchungaji Mackenzie akiendeleza mafunzo ya kupotosha kwenye shamba hilo.
Mwanamume huyo alijitambulisha kama Zablon Mwana wa Yesu, msaidizi wa Paul Mackenzie.
Hatimaye babake mwanamume huyo amezungumza na jarida la Nation na alisema kwamba kijana yake alianza kuonesha tabia zisizo za kawaida mpaka kupelekea kuiasi familia yake mwaka 2016 alipofuata Mackenzie.
Kwao ni Butere kaunti ya Kakamega.
Mzee Cleophas Lihoywa alisema kuwa tangu kipindi hicho, hakuwahi kupokea taarifa zozote kutoka kwa mwanawe na kusema kuwa hatua ya kujiita Zablon wa Yesu ni kumdhihaki Mungu.
Mzee huyo aliambia jarida hilo kwamba yuko radhi mwanawe kufungwa maisha jela endapo hatokubali kuasi mafunzo ya Mackenzie na kurudi nyumbani kwa mke wake na watoto wake wane.
"Jina lake rasmi ni Zablon Atanda na sio jina hilo mnalosikia," alisema.
Mzee huyo aliiomba serikali kumpa nafasi ya pili kijana wake kwani alikuwa mtu mzuri na iwapo hatobadili mienendo baso apewe adhabu ya kifungo cha maisha jela.
"Natoa wito kwa serikali kufikiria kumsamehe ikiwa inaona mantiki na kuomba radhi kwa kutumia vibaya maandiko na kusababisha mauaji makubwa ya raia wasio na hatia," alisema.