Idadi ya maiti zilizofukuliwa Shakahola imepita 200 huku zaidi ya watu 600 wakiendelea kutafutwa!

Kamishna wa polisi eneo la Pwani Jumamosi baada ya ufukuzi wa maiti 22 zaidi alisema mtu mwingine anayehusishwa na Mackenzi alitiwa mbaroni.

Muhtasari

• Kamishna wa eneo la pwani alisema watu 610 mpaka sasa wameripotiwa kutojulikana waliko na familia zao.

• Aliongeza kuwa sampuli 93 za DNA zimekusanywa na kwamba waathiriwa 14 wameunganishwa tena na familia zao.

MCHUNGAJI PAUL MACKENZIE
Image: ALPHONSE NGARI

Shughuli ya ufukuzi wa maiti katika kaunti ya Kilifi shamba la Shakahola la mchungaji mwenye itikadi potovu Paul Mackenzie ilirejelewa mapema wiki jana na mpaka sasa idadi ya maiti zilizofukuliwa kijumla imepita 200.

Kufikia Jumamosi jioni, maafisa wa DCI wanaoendesha shughuli hiyo katika shamba lenye ukubwa wa ekari 800 walifukua maiti 22 zaidi na kufanay idadi hiyo kuzidi 200.

Idadi hiyo inaendelea kunenepa mithili ya puto linalopuliziwa hewa ndani yake kila uchao huku familia nyingi zikiwa zimekita kambi eneo hilo wakiwa na Imani ya kupata wapendwa wao waliotoweka nyumbani wakidaiwa kujiunga na kanisa la Mackenzie miaka michache iliyopita.

Baada ya kufukuliwa kwa miili 22 zaidi Jumamosi, kamishna wa eneo la Pwani Rhoda Onyancha alisema kwamba mtu mwingine mmoja anayeshukiwa kuwa mwanachama wa Mackenzie alitiwa mbaroni na kufichua kwamba taarifa walizo nazo ni kuwa takribani watu 610 wameripotiwa kutojulikana waliko huku shughuli hiyo ikiendelea.

Aliongeza kuwa sampuli 93 za DNA zimekusanywa na kwamba waathiriwa 14 wameunganishwa tena na familia zao.

Onyancha pia alisema ili kupanga upya usaidizi huo wa vifaa, ufukuaji huo ulikuwa umesitishwa kwa siku mbili, kuanzia Jumapili, Mei 12, hadi Jumanne, Mei 16. Hata hivyo, jitihada za kutafuta na kuokoa zinaendelea.