Jiwe ladondoka kutoka ghorofa ya 10 na kumuua mvulana wa miaka 2 kitandani

Mtoto huyo alikuwa amelala kitandani wakati jiwe lilidondoka kutoka ghorofa ya 10 ya mjengo jirani unaoendelea kujengwa. Jiwe lilimpata kichwani na kifuani na kumuua papo hapo.

Muhtasari

• Ukuta wa mjengo huo unaoendelea kujengwa uliporomoka na mawe 20 yakaangukia nyumba jirani.

• Kwa bahati mbaya, jiwe moja liliangukia paa la chumba ambacho mtoto alikuwa amelala na kumuua papo hapo.

Mtoto wa miaka 2 amefariki baada ya kuangukiwa na jiwe kichwani mtaani Eastleigh.
Mtoto wa miaka 2 amefariki baada ya kuangukiwa na jiwe kichwani mtaani Eastleigh.
Image: Malazi ya mtoto marehemu mtaani Eastleigh aliyefariki baada ya kuangukiwa na jiwe kichwani

Wazazi katika mtaa wa Eastleigh wanaomboleza mwanawe, mvulana wa miaka miwili ambaye aliripotiwa kufariki baada ya kuangukiwa na jiwe kutoka kwa ghorofa ya kumi ya jingo jirani ambalo lilikuwa linaendelea kujengwa.

Wazazi wa mvulana huyo waliiambia runinga ya Citizen kwamba mwanao alikuwa amelala baada ya jiwe kutoka jingo jirani ambalo linaendelea kujengwa kuanguka na kumpata kitandani na kumuua papo hapo.

Mtoto huyo alikuwa amejilaza katika kitanda chake akitazama vibonzo kwenye runinga kabla ya mkasa ambapo jiwe hilo lilishuka kwa kishindo cha aina yake na kuvunja mabati hadi kumpata.

Wakaazi walisema kuwa walijaribu kumpigia mwenye jumba  linaloendelea kujengwa lakini alizima simu.

“Tumepiga simu kwa mwenyewe lakini akazima, tumeripoti kwa polisi na wamefika wakachukua hilo jiwe na kuenda nalo,” Kelvin Nyaga, msimamizi wa kazi hiyo ya mjengo alisema.

Ripoti ya Citizen ilisema kwamba upande wa ukuta wa jingo hilo ambalo lilikuwa limefika ghorofa ya kumi uliporomoka na mawe kuanguka pande tofauti, mengi yao yakikuta majumba ambapo yalikuwa chini mkabala na ghorofa hiyo.

Ukuta mzima ambapo ulikuwa kama na mawe 20 uliporomoka na kwa mtoto huyo, jiwe lilimpata kichwani na kifuani na kumuua.

Wakili wa familia hiyo, George Omwansa alisema kuwa watamchukulia hatua za kisheria mwenye jumba hilo.

 Ujenzi wa jingo hilo ulisitishwa mara moja na polisi wa kituo cha Pangani wakimtaka mmiliki wa jingo hilo kujisalimisha kituoni hapo mara moja.

Ilibainika kwamba si mara ya kwanza kuta za jingo hilo kuporomoka kwani wakati mmoja pia ziliporomoka na kuharibu magari yaliyokuwa yameegeshwa chini.