Video: Pasta Mackenzie awaomba wanahabari kumnunulia mkate na maziwa

Mchungaji huyo aliwaambia wanahabari kwamba wamepata pesa nyingi kutokana na kuangazia habari zake na kama njia ya kurudisha shukrani, wangemnunulia angalau mkate.

Muhtasari

• Mchungaji huyo aliyeonekana kuzungumza kwa ucheshi aliwaambia wanahabari kwamba ni wajibu wao kumpa mkate na maziwa kwa sababu maudhui yake yamewaingizia kipato kikubwa.

Mackenzie aomba mkate na maziwa kutoka kwa wanahabari.
Mackenzie aomba mkate na maziwa kutoka kwa wanahabari.
Image: Screengrab

Mhubiri tata Paul Mackenzie wa kanisa la Good News International amewashangaza wanahabari baada ya kuwataka kumnunulia mkate na maziwa angalau kama njia moja ya kurudisha shukrani kutokana na kile alisema kuwa wamepata hela ndefu sana kutokana na kuangazia taarifa na habari zake na msitu wa Shakahola.

Mackenzie ambaye aliwasilishwa mahakamani siku ya Ijumaa baada ya kuwa rumande kwa siku 30 anakabiliwa na mashtaka mbalimbali yakiwemo ya mauaji ya halaiki ambao walifariki na kuzikwa katika makaburi ya jumla huko Shakahola baada ya kusemekana kuwa Mackenzie alikuwa anawarai kujinyima chakula na maji ili kumuona Mungu.

Kaitka ombi lake kwa wanahabari, Mackenzie alisema kuwa amefungiwa na hana uhuru wa kujipatia pesa na hivyo ingekuwa jambo la busara kwa wanahabari hao kumnunulia mkate na maziwa.

“Mmeunda pesa nyingi sana lakini hamwezi ninunulia hata mkate. Mimi nimekaziwa siwezi kupata hata pesa. Si mwende mniletee angalau na pakiti ya maziwa bana. Angalau bana mimi niko ndani wewe uko nje, ama namna gani bwana,” Mackenzie aliwaambia wanahabari hao katika klipu ya video ambayo imeibuliwa.

Itakumbukwa kuwa mchungaji huyo mwenye utata anaandamwa na tuhuma za kuwarai waumini wake kujitesa njaa ya maji na chakula hadi kufa katika kile alikuwa anawaaminisha kuwa ndio njia pekee na sahihi ya kukutana na Mungu.

Kufikia sasa, Zaidi ya maiti 240 zimefukuliwa katika shamba la Shakahola lenye upana wa ekari 800 na wikendi iliyopita akiongea katika ibada ya kanisa huko Kirinyaga, waziri wa usalama wa ndani profesa Kithure Kindiki alisema kuwa awamu ya tatu ya kufukua maiti kwenye shamba hilo itang’oa nanga Leo Jumatatu.