Babu Owino aeleza kwa nini wabunge wengi wa Azimio hawakuwepo bungeni

Usiku wa Jumatano, jumla ya wabnge 257 walipiga kura, huku wabunge 176 wakipiga kura ya ndio na wabunge 81 wakipiga kura ya hapana.

Muhtasari

Owino alisema kuwa alikuwa na kesi dhidi yake katika mahakama ya Milimani Leo Alhamisi na hivyo alifaa kukutana na wakili.

Babu Owino aelezea kwa nini wabunge wa Azimo hawakuhudhuria kikao cha kupigia kura mswada wa fedha 2023.
Babu Owino aelezea kwa nini wabunge wa Azimo hawakuhudhuria kikao cha kupigia kura mswada wa fedha 2023.
Image: Facebook

Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino ameelezea sababu kuu iiyowafanya wabunge wengi wa upinzani kutokuwepo bungeni wakati wa upigaji kura kwa mswada wa fedha 2023 usiku wa Jumatano.

Owino ambaye pia hakuwepo bungeni licha ya kuwa katika mstari wa mbele kuapa kupiga kura ya kuangusha mswada huo, alifanya klipu fupi ambapo alielezea sababu zake na wenzake kukosekana bungeni.

Kulingana na Babu Owino, spika wa bunge Moses Wetang’ula alikuwa amedokeza kwamba kura za kuupitisha au kuuangusha mswada huo zingefanyika Jumanne wiki kesho na hivyo alimuona kiongozi wa wachache bungeni Opiyo Wandayi kumruhusu kuondoka ili kwenda kukutana na wakili wake.

Owino alisema kuwa alikuwa na kesi dhidi yake katika mahakama ya Milimani Leo Alhamisi na hivyo alifaa kukutana na wakili wake ili kuandaa faili za utetezi wake.

“Leo nilienda bungeni tayari kwa kujadili mswada wa fedha 2023 na mida ya saa tano asubuhi, spika alipitisha kwamba mjadala ungeendelea hadi usiku saa tatu na kisha kuendelea Jumanne wiki kesho ambapo upigaji kura ungefanyika. Kulingana na maelezo hayo, nilimfuata mheshimiwa Opiyo Wandanyi nikamuomba ruhusa kuondoka ili kukutana na wakili wangu, kesi yangu imeratibiwa Alhamisi,” Owino alisema.

Kulingana naye alishangaa sana kuona spika akiamrisha upigaji kura kufanyika usiku huo wa Jumatano, licha ya kwamba wengi wa wabunge hawakuwepo.

“Nikiwa katka ofisi ya wakili wangu niligundua kwamba spika alibadilisha maelewano ya awali na kupitisha kwamba upigaji kura ungefanyika Leo. Kufikia wakati huo, wabunge wengi walikuwa wameamini kwamba upigaji kura ungefanyika baada ya Jumanne wiki kesho. Na hilo linaeleza ni kwa nini wabunge wengi walikosa kuhudhuria, haswa kutoka mrengo wa Azimio,” alisema.

Usiku wa Jumatano, jumla ya wabnge 257 walipiga kura, huku wabunge 176 wakipiga kura ya ndio na wabunge 81 wakipiga kura ya hapana.