Rais Ruto ametoa hakikisho kwamba kila Mkenya ambaye atapanda miti kwenye shamba lake atalipwa na serikali katika miaka michache ijayo.
Akizungumza katika siku ya kuadhimisha vyama vya ushirika yaani saccos kaitka ukumbi wa KICC jijini Nairobi Jumamosi Julai mosi, rais alisema kuwa tayari yeye ameanza kujipanga mapema kwa kupanda miti kwenye mashamba yake.
Aliwataka Wakenya wengine kukumbatia mpango huo ili ikija kufika wakati wa serikali kuwalipa wenye miti shambani, wasije wakalia wakisema kuwa hawakuwa wanajua.
"Nataka niwape kongole na kuwajulisha kuwa siku za usoni, baada ya miaka michache, utalipwa kwa kuwa na miti shambani kwako. Kwa hiyo anza kujiandaa tayari nimeshajiandaa na kuanza kupanda miti. Na mimi sitaki mtu aseme sikuwapa taarifa kila mtu aanze kupanda miti maana miti ni biashara ya siku za usoni, sio kuuza miti, hapana, utalipwa tu kwa kuwa na miti shambani kwako. Kwa hivyo huu ndio mpango, tupande miti," rais Ruto alisema.
Ikumbukwe hii si mara ya kwanza kwa kiongozi huyo wa taifa kuonekana waziwazi akipigia debe upandaji miti kama njia moja ya kuzuia na kudhibiti mabadiliko ya tabia ya hali ya nchi.
Mwaka jana baada ya kuapishwa, alisema kuwa serikali yake ifikapo mwaka 2032, anataka iwe imepanda miti Zaidi ya bilioni 15 ili kuzuia ukame ambao umekuwa ukiramba maeneo mengi ya nchi na hivyo kusababisha njaa kwa mamilioni ya Wakenya kila mwaka.
Pia aliwahi nukuliwa akisema kuwa serikali haswa ya kaunti ya Nairobi ingewapa kazi wale vijana waliokuwa wanafanya kazi mtaani, kibarua cha kupanda miti katika kaunti hiyo ambayo ni kitovu cha uchumi wa Kenya.