Malala afichua sababu ya kuhudhuria mikutano ya Mawaziri

Alisema akiwa Katibu Mkuu wa chama hicho, hana budi kuhakikisha yote ambayo rais aliahidi Wakenya wakati wa kampeni yanaafikiwa

Muhtasari
  • Mugane alitaja kujumuishwa kwa Malala na wengine watatu katika mkutano huo kuwa ni kinyume cha katiba.
Seneta wa Kakamega Cleopas Malala
Image: MAKTABA

Katibu Mkuu wa United Democratic Alliance (UDA) Cleophas Malala amesema ataketi katika Baraza la Mawaziri ili kuhakikisha kuwa manifesto ya Rais William Ruto inatekelezwa vyema.

Alisema akiwa Katibu Mkuu wa chama hicho, hana budi kuhakikisha yote ambayo rais aliahidi Wakenya wakati wa kampeni yanaafikiwa ndani ya miaka hii mitano.

"Kama kiongozi, rais anapaswa kutimiza kile alichoahidi kwenye kampeni na ni jukumu langu kuhakikisha hilo linafanyika kwa kuwa sehemu ya Baraza la Mawaziri," Malala alisema.

Uwepo wake katika kikao cha Baraza la Mawaziri ulikuwa umepingwa na wakili Charles Mugane.

Mugane alitaja kujumuishwa kwa Malala na wengine watatu katika mkutano huo kuwa ni kinyume cha katiba.

Wengine watatu ni washauri wa rais David Ndii (Uchumi), Monica Juma (Usalama wa Kitaifa) na Harriette Chiggai (Haki za Wanawake).

Kesi hiyo itatajwa Septemba 20 kwa maelekezo zaidi.

Katibu mkuu wa UDA alikuwa akizungumza huko Sabatia, Kaunti ya Vihiga, ambapo Gavana Wilber Ottichilo alikuwa akiagiza usambazaji wa mbolea kwa kaunti zote tano ndogo.

Kaunti hiyo ilikuwa imepokea mbolea ya ruzuku kutoka kwa serikali ya Kitaifa.

Sambamba na hilo, gavana wa Vihiga aliitaka serikali na upinzani kufanya kazi pamoja kwa ajili ya uchumi wa nchi.

"Uchumi wetu kwa sasa uko katika hali mbaya na ni wakati wa kufanya kazi ili kuufufua na hilo linaweza kuafikiwa tu ikiwa tutaweka tofauti zetu kando kama viongozi," Ottichilo alisema.

Maoni yake yaliungwa mkono na viongozi wengine waliokuwepo wakiongozwa na Mbunge wa Sabatia Clement Sloya.