Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja ametoa wito kwa rais William Ruto kufufua mradi wa Kazi Mtaani uliositishwa pindi baada ya kuingia madarakani mwaka mmoja uliopita.
Akizungumza Jumanne, Sakaja alimuomba Ruto kufufua mradi huo uliotoa maelfu ya ajira kwa vijana wasio na kazi kama njia moja ya kupunguza ujambazi haswa katika kaunti ya Nairobi.
Kulingana na Sakaja, vijana wengi wasio na kazi wanalazimika kuingilia vitendo vya ujambazi ili kujipatia riziki, na hivyo ni bora kwa serikali kurudisha mradi huo wa kuwapa vijana ajira.
Gavana huyo aidha alipiga upato mradi wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu akisema kwamba utatoa kazi kwa vijana na kina mama pia.
“Hatuwezi andika kazi kila mtu kwa kaunti, kazi yetu ni kujenga biashara ambazo zitatoa ajira kwa vijana wetu. Ndio maana runashukuru mpango wa ujenzi wa nyumba, vijana mtapata kazi hapo, akina mama mtapika hapo. Kazi mtaani vile ilikuwa, ujambazi ulikuwa umepungua kwa asilimia 47. Na ndio maana tunaomba rais Ruto huo mradi urudi na kama itarudi kwa njia hiyo tuingie kwa kazi ile ambayo itapatikana ya kupanda miti na kujenga nyumba,” Sakaja alisema.
Pindi baada ya kuapishwa mwaka jana mwezi Septemba, Ruto alisema kwamba mradi wa kazi mtaani ulisitishwa na baadae akaahidi kwamba vijana wote waliokuwa wameandikwa kazi mtaani watapewa ajira ya kupanda miti katika maeneo mbali mbali katika kaunti ya Nairobi.
Inasubiriwa kuonekana kama rais Ruto atasikia kilio hicho cha gavana wa Nairobi ambaye amesakamwa na shinikizo kutoka kwa maelfu ya vijana waliomchagua wakimtaka kuwapa kazi ili kujikimu wakati huu ambao uchumi unazidi kuzorota na hali ya maisha kuwa ngumu.