Seneta Ledama Olekina ampa kazi msichana jasiri aliyewasuta viongozi Uasin Gishu

Msichana Mercy Tarus aliwapa makavu bila kupepesa jicho viongozi hao baada ya kufika kwa kuchelewa kwenye mkutano ulionuiwa kuwakutanisha wahanga wa mradi uliogeuka skendo kuhusu elimu Finland.

Muhtasari

• Kuwasuta kwake mbele ya macho yao kuliwavutia Wakenya wengi kwa jinsi msichana huyo mhitimu alivyowapa makavu ana kwa ana bila kuwaficha.

• Mercy Tarus ni miongoni mwa vijana wahitimu ambao walirambwa kwenye skendo kubwa.

Olekina kumpa kazi Mercy Tarus
Olekina kumpa kazi Mercy Tarus
Image: Twitter, Maktaba

Seneta wa Narok Ledama Olekina amejitokeza na kusema kwamba yuko tayari kukutana na binti Mercy Tarus ili kumpa kazi.

Mercy Tarus mapema wiki hii aligonga vichwa vya habari baada ya kuwasuta vikali viongozi wa kaunti ya Uasin Gishu – seneta wa sasa ambaye ni gavana wa zamani Jackson Mandago, gavana wa sasa Jonathan Bii Chelilim na naibu gavana Barorot miongoni mwa wengine.

Kuwasuta kwake mbele ya macho yao kuliwavutia Wakenya wengi kwa jinsi msichana huyo mhitimu alivyowapa makavu ana kwa ana bila kuwaficha.

Ni kutokana na ari hii ambapo seneta Olekina amejitolea kumpa kazi akisema kwamba kesho angavu ni ya vijana wenye ujasiri kama wa kwake.

“Mercy Tarus Ningependa unifanyie kazi… sema moyo wako … wakati ujao ni wa vijana waaminifu! Hebu tuzungumze,” Olekina alimwambia kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Mercy Tarus ni miongoni mwa vijana wahitimu ambao walirambwa kwenye skendo kubwa ambayo imekuwa ikizua mjadala mkali mitandaoni na amabyo ilifanyika katika kaunti ya Uasin Gishu chini ya uongozi wa seneta wa sasa.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, kaunti hiyo iliwahadaa wqzazi kutoa mamilioni ya pesa kwa ajili ya serikali kuwasaidia katika kuwapeleka wanao kujiendeleza kimasomo nchini Ufini, lakini hilo halikutokea, na wachache waliokwenda Ufini waliishia kuhangaika na kufukuzwa masomoni kwa kutolipiwa ufadhili wa masomo kama ambavyo kaunti ilivyowaambia wazazi.

Katika video moja, msichana huyo alionekana akiwauliza maswali magumu viongozi hao ambao walifika katika mkutano uliowakutanisha wazazi wahanga na watoto wao, katika mbinu na kutafuta suluhisho la kudumu kwa sakata hilo ambalo sasa limeenea pakubwa hadi nje ya nchi.