Raila ataandikishwa kwenye mpango wa 2k pesa za wazee kila mwezi DP Gachagua

"Na tukiandikisha hao nimemwambia PS huyu mzee wa kitendawili [Raila Odinga] umwandikishe akuwe anachukua elfu yake mbili kila mwezi ndio aende kupumzika,” Gachagua

Muhtasari

• Upande wa Serikali umeanzisha malumbano upya na upinzani kisa tamko la Odinga kuhusu balozi wa Marekani humu nchini Meg Whiteman.

• Ruto mapema Ijumaa alimtaka Odinga kuwa na heshima akisema kwamba hafai kumuita Whiteman kama tapeli hali ya kuwa yeye ndiye tapeli mkuu wa kisiasa.

Gachagua amshambulia Odinga tena
Gachagua amshambulia Odinga tena
Image: Maktaba

Naibu rais Rigathi Gachagua ametupa makombo katika uso wa kinara wa Azimio Raila Odinga kwa kusema kwamba Odinga ameshafiisha umri wa kupokea pesa za wazee za kila mwezi.

Akizungumza katika kaunti ya Uasin Gishu Ijumaa alasiri, Gachagua alisema kwamba hivi karibuni serikali itaanzisha mpango wa kuandikisha wazee wengine ambao wamehitimu umri wa miaka 70 kwenda mbele ambao watakuwa wananufaika kwa shilingi elfu mbili kila mwezi.

Akionekana kumkejeli Odinga, Gachagua alisema kwamba hata Odinga – mwenye umri wa miaka 78 – anastahili kuandikishwa katika mpango huo ili awe akipokea kilicho chake kila mwezi kama njia moja ya kumpumzisha nyumbani badala ya kile alisema kwamba anasumbua serikali ya Ruto.

“Rais ametuagiza tuanzishe tena kuandikisha wazee wa miaka 70 kwenda juu waanze kupata marupurupu yao. Na tukiandikisha hao nimemwambia PS huyu mzee wa kitendawili [Raila Odinga] umwandikishe akuwe anachukua elfu yake mbili kila mwezi ndio aende kupumzika,” Gachagua alisema huku watu wakimshangilia.

Upande wa serikali umeanzisha upya mashambulizi dhidi ya mrengo wa upinzani haswa kinara wao Raila Odinga siku moja baada ya kukashifu matamshi ya balozi wa Marekani humu nchini Meg Whiteman.

Wakati wa kongamano la ugatuzi Eldoret Jumatano, Whiteman ambaye alikuwa na rais Ruto alipongeza Kenya na kusema kuwa ndilo taifa lenye ustawi wa kipekee barani Afrika huku pia akisema kuwa matokeo ya urais wa mwaka jana yalikuwa ya uwazi, haki na kweli.

Odinga Alhamisi katika kongamano hilo alisuta matamshi hayo akimtaka Whiteman kufyata ulimi wake na kujitenga mbali na masuala ya humu nchini la sivyo waanzishe mchakato wa kusababisha kurudishwa kwake nchini kwao Marekani.

Odinga alimtaja balozi huyo kama tapeli.

Ijumaa rais Ruto amemtaka Odinga kumheshimu Whiteman akisema kuwa kati yake na Whiteman Odinga ndiye anafaa kuitwa tapeli na katili na wala si balozi huyo.