Mganga wa kienyeji na mkewe mbaroni baada ya mgonjwa kufariki kilingeni

Kulingana na msemaji wa polisi, Bateganya Bwiga, 62 alikamatwa pamoja na mkewe, Madina Baseke, 70 baada ya Margaret Nantale, 53 kufariki katika kilinge chao.

Muhtasari

• Alibainisha kuwa hali ya Nantale ilizidi kuzorota, mganga huyo na mkewe walikataa kumpeleka hospitalini.

HISANI
Image: Vifaa vya uchawi.

Polisi katika wilaya ya Bugweri mashariki mwa Uganda wamemkamata mganga mmoja na mkewe baada ya mwanamke mmoja ambaye aliletwa katika kilinge chao kwa matibabu kufariki, jarida la Nile Post limeripoti.

 Kulingana na msemaji wa polisi nchini humo, Fred Enanga, Bateganya Bwiga, 62 alikamatwa pamoja na mkewe, Madina Baseke, 70 baada ya Margaret Nantale, 53 kufariki katika kilinge chao katika kijiji cha Budubye, kata ndogo ya Buyanga wilayani Bugweri.

"Mganga wa kienyeji alisababisha uhamisho wa Nantale kutoka kwa kilinge cha Obara hadi kwenye kilinge chake na kumhudumia kwa siku tatu. Waliendelea kumzuilia mwathiriwa katika kilinge chao hata hali yake ilipokuwa mbaya badala ya kumpeleka hospitali kwa matibabu zaidi,” Enanga alisema.

Alibainisha kuwa hali ya Nantale ilizidi kuzorota, mganga huyo na mkewe walikataa kumpeleka hospitalini kwa matibabu bali walimweka kwenye kilinge chao kwa siku tatu hadi alipofariki.

Enanga alisema washukiwa hao wawili wanakabiliwa na mashtaka yanayohusiana na uzembe wa uhalifu na kusababisha kifo cha mtu.