Sifuna afichua sababu ya kuacha kazi iliyokuwa ikimlipa 400,000 kwa mwezi

Baada ya kuacha kazi hiyo, Sifuna alisema alihamia kazi ya kibinafsi kama mwanasheria.

Muhtasari

•Alisema alipopata kazi hiyo alifurahi kwani alikuwa ametoka tu kupanda daraja kutoka kazi inayolipa Sh40,000 hadi mpya ikimlipa Sh150,000.

•"Nilikuwa nalipwa Sh400,000 mwaka 2013. Zilikuwa pesa nzuri, lakini nilijiuliza ni nini hitaji la msongo wote wa mawazo," alisema.

b6251efb2cdb00bc
b6251efb2cdb00bc
Image: MAKTABA

Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna amefichua kuwa aliwahi kuacha kazi iliyomlipa Sh400,000 kila mwezi ili kulinda afya yake ya akili.

Seneta huyo alizungumza katika mahojiano na TV47 Ijumaa usiku.

Sifuna alisema alipopata kazi hiyo kwa mara ya kwanza kama meneja wa masuala ya sheria katika kampuni ya matangazo, alifurahi kwani alikuwa ametoka tu kupanda daraja kutoka kazi inayolipa Sh40,000 hadi mpya ikimlipa Sh150,000.

Alisema kampuni hiyo hata ililipia gari lake la kwanza.

"Wakati mwingine nasikia watu wakisema kazi ni kazi. Kazi si kazi. Kuna kazi ambayo inaweza kubadilisha maisha yako pamoja na familia na kijiji chako na kuna kazi ambayo inasumbua afya yako ya akili," alisema.

Sifuna alisema kazi hiyo ilikuwa ya mabadiliko kwake kwani alihama kutoka makao ya watumishi hadi nyumba ya vyumba vitatu.

Lakini madhara ya kazi hiyo alisema, ni kwamba alikuwa na 'bosi kutoka kuzimu'.

“Najua ananiangalia kwa sababu ni rafiki yangu siku hizi, alikuwa akinipa presha kubwa, ilipofika 2013 nilijiambia hii kazi si afya kwangu.

Nilikuwa nalipwa Sh400,000 mwaka 2013. Zilikuwa pesa nzuri, lakini nilijiuliza ni nini hitaji la msongo wote wa mawazo,.

Siku nilipoacha kazi hiyo, kwa mara ya kwanza nililala huku simu yangu ikiwa imezimwa kwa sababu bosi wangu alikuwa akipiga simu muda wowote kunipa kazi. Nililala kama mtoto mchanga. Nilikuwa nimezoea kulala na simu yangu chini ya mto kwa sababu ya kazi hiyo." Alisema.

Baada ya kuacha kazi hiyo, Sifuna alisema alihamia kazi ya kibinafsi kama mwanasheria.

Alisema wakati huo, uchumi ulikuwa mzuri na vyama na watu waliokuwa wakinunu ardhi walikuwa wateja wake. Kampuni nyingi pia zilikuwa zikisajiliwa wakati huo na zilihitaji usaidizi wa mwanasheria.

Sifuna alisema alijiwekea lengo la kutengeneza Sh50,000 kwa mwezi kutokana na shughuli zake za kibinafsi, ambazo zilitosha kulipa kodi yake na mafuta ya gari lake.

"Niliweza kujiendeleza kwa muda," Seneta alisema.

Sifuna alisema kwa sababu alikuwa na wakati mwingi wa kupumzika katika kazi ya kibinafsi, alipata njia yake katika siasa.

Alikumbuka kuwa alikutana na kiongozi wa Azimio Raila Odinga alipokuwa bado chuoni, lakini alikutana na Raila ofisini kwake kwa mara ya kwanza mnamo 2013.