Ruto adai kuna shilingi 50b zenye hazina kazi na zimelala tu bure kwenye makasha ya CBK

Kiongozi huyo wa nchi aliwaomba magavana kwa unyenyekevu kukubali kutumia pesa hizo katika kaunti zao ili kumwezesha kukusanya ushuru zaidi.

Muhtasari

• Ruto aliwaomba magavana wa kaunti zote 47 kwa unyenyekevu kutumia pesa hizo ili kuvutia miradi mingi ya maendeleo katika kaunti ambazo wanaongoza.

RUTO
RUTO
Image: X

Rais William Ruto amewasihi magavana kutoogopa kutumia pesa zipatazo shilingi bilioni 50 ambazo zimezembea tu bure katika rafu za benki kuu ya Kenya ili kufanya maendeleo katika kaunti zao.

Akizungumza wakati wa Mkutano wa Kilele wa Hali ya Hewa barani Afrika 2023 mnamo Jumanne, Septemba 5, mkuu huyo wa nchi alifichua kuwa pesa hizo hazifanyi kazi katika Benki Kuu ya Kenya (CBK) na zinatafutiwa kazi ya kufanya.

Ruto aliwaomba magavana wa kaunti zote 47 kwa unyenyekevu kutumia pesa hizo ili kuvutia miradi mingi ya maendeleo katika kaunti ambazo wanaongoza.

“Ombi la mwisho ambalo ningependa kutoa kwa magavana wangu, kama mnavyojua mabibi na mabwana, wakati kuna pesa huwa nafanya kadri ya uwezo wangu kuachia pesa hizo kwenu. Nyinyi ni mashahidi hata kama hamtaki kukubali, lakini sasa niko na changamoto nyingine, kwa sababu watu wengi sasa wananiambia kwamba ninawaharibu magavana na pesa nyingi. Kwa sababu hivi ninavyoongea na nyinyi kuna shilingi bilioni 50 za Kenya ambazo hazina kazi katika kasha la Benki Kuu ya Kenya. Ombi langu kwenu ni tafadhali tumieni hizi pesa,” Rais aliwaambia magavana.

“Endapo mtatumia hizi pesa kikamilifu tutakuwa na Wakenya wengi ambao watakuwa wasambazaji, waonozaji wa programu na wengine… na sasa nitaenda kuwaongeza pesa zingine, kwa hiyo ombi langu kwenu ni kwamba acha tuhakikishe kwamba tunazindua miradi, tunatumia hizi hela na hivyo ndivyo tunainua uchumi wetu na pia mimi nitakuwa na uwezo wa kukusanya ushuru Zaidi ili kwamba niweze kufanya chenye nahitaji kufanya,” aliongeza mkuu wa taifa.

Wakenya wengi walitoa maoni tofauti kuhusu matamshi hayo ya rais, wengine wakisema ni mwelekeo mzuri kwa kaunti huku wengine wakikumbuka matamshi ya serikali kuhusu uchumi uliodorora.