Serikali ilimnyima Raila kibali cha kuhudhuria ACS lakini AU na UN wakasisitiza awepo - Etale

Etale alisema kuwa kutokana na uingiliaji kati wa AU na UN, ndio sababu ya katibu katika wizara ya usalama wa ndani Raymond Omollo alilazimika kutoa barua nyingine akielezea mabadiliko katika itifaki.

Muhtasari

• Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Etale alizua kwamba ilibidi UN na AU waingilie kati na kuishrutisha serikali kumpa kibali.

Ruto na Gachagua
Ruto na Gachagua
Image: X

Mkurugenzi wa  mawasiliano katika chama cha ODM Philip Etale amezua madai kwamba serikali kupitia wizara ya mazingira ilikuwa imemnyima kiongozi wa upinzani Raila Odinga kibali cha kuhudhuria mkutano wa kilele cha kujadili hali ya hewa unaofanyika katika ukumbi wa KICC jijini Nairobi.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Etale alizua kwamba ilibidi UN na AU waingilie kati na kuishrutisha serikali kumpa kibali.

Etale alisema kuwa kutokana na uingiliaji kati wa AU na UN, ndio sababu ya katibu katika wizara ya usalama wa ndani Raymond Omollo alilazimika kutoa barua nyingine akielezea mabadiliko katika itifaki ya wale ambao wangeruhusiwa kuingia KICC kwa ajili ya mkutano huo.

“Bw. Raymond Omollo ameamua kutoa taarifa… hofu ya Baba. Kumbuka Wizara ya Mazingira ilikataa kumpa kibali lakini AU na UN walisema ni LAZIMA Baba ahudhurie Mkutano huu muhimu sana,” Etale alisema.

Omollo katika barua aliyoipakia kwenye mtandao wa X awali ukijulikana kama Twitter, alieleza mabadiliko yaliyofanyiwa itifaki kwa wageni mbali mbali waliodhuhuria mkutano huo ambao umeng’oa nanga Jumatatu na unatarajiwa kukamilika leo Jumatano.

Baada ya kufika katika ukumbi wa KICC ikiwa ni siku ya pili ya mkutano huo muhimu wa kujadili mabadiliko ya tabia ya nchi, Odinga alionekana kukaribishwa na naibu wa rais Rigathi Gachagua ambapo walisalimiana kwa tabasamu kuu kwenye nyuso zao.

Wawili hao ambao wamekuwa wakipapurana kwenye mikutano ya kisiasa nchini kwa muda sasa waliweka tofauti zao za kisiasa kando na kujumuika pamoja katika mkutano huo unaolenga kutafuta mbinu mbadala za kutatua madhara ya mabadiliko ya tabia ya nchi kote duniani.