Rais Ruto amkaribika kwenye ikulu ya Nairobi mtetezi wake mkali Cosmo Choi

Baada ya kukutana na Ruto katika ikulu ya Nairobi, Choi alionesha furaha yake akisema kwamba hatimaye amefanikiwa kuonana na kiongozi huyo, ikiwa ni mara ya pili kuonana naye tangu awe rais.

Muhtasari

• “Nikiwa na Amiri Jeshi Mkuu (C-in-C) Rais Dkt Bill William Ruto katika Ikulu nilipomtembelea mapema leo." - Choi.

Cosmo Choi na Ruto.
Cosmo Choi na Ruto.
Image: Facebook

Mtetezi mkali wa sera za rais William Ruto kwa muda mrefu, Cosmo Choi hatimaye amekutana na kiongozi huyo wa taifa katika ikulu ya Nairobi.

Choi ambaye yuku humu nchini kwa wiki kadhaa baada ya kurudi nyumbani kutoka Marekani kwa likizo ya muda alijizolea umaarufu mkubwa haswa mwaka jana kipindi cha kampeni za kuelekea katika uchauzi mkuu.

Choi alikuwa mmoja kati ya watu waliokuwa wakimpigia debe vikali kiongozi huyo ambaye kipindi hicho alikuwa naibu rais aliyekuwa haonani jicho kwa jicho na rais wa kipindi hicho Uhuru Kenyatta.

Baada ya kukutana na Ruto katika ikulu ya Nairobi, Choi alionesha furaha yake akisema kwamba hatimaye amefanikiwa kuonana na kiongozi huyo, ikiwa ni mara ya pili kuonana naye tangu awe rais.

“Nikiwa na Amiri Jeshi Mkuu (C-in-C) Rais Dkt Bill William Ruto katika Ikulu nilipomtembelea mapema leo. Mimi Cosmas Choi Kipchumba mwenyewe naidhinisha ujumbe huu 💯 %,” aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook akiambatanisha na picha za wawili hao wakisalimiana kwa furaha na tabasamu ghaya.

Mara ya kwanza kukutana na Ruto ilikuwa ni kule Marekani miezi michache baada ya kuapishwa mwezi Septemba mwaka jana.

Ruto alikwenda katika kongamano Marekani na baadae alikutana na Wakenya wanaoishi katika taifa hilo lenye nguvu duniani, Choi akiwa mmoja wao.