Kalonzo alikuja ikulu usiku nikamuona anafurahia chakula na supu - DP Gachagua

"Kalonzo amekuja pale na amekula chakula, amefungwa kitambaa hapa [kiunoni] cheupe amekula vizuri si huyo ndio wa kufukuzwa? aliuliza naibu rais.

Muhtasari

• "Kama watu lazima wafukuzwe kwa kukutana na rais, mbona huyu Kalonzo na alikuwa pale siku tulikuwa na marais wa Afrika" - Gachagua alisema.

Gachagua na Kalonzo.
Gachagua na Kalonzo.
Image: Facebook

Naibu wa rais Rigathi Gachagua amezua vichekesho baada ya kuhadithia jinsi alimuona kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka akifurahi kula chakula katika ikulu ya Nairobi mapema wiki hii.

Kwa mujibu wa Gachagua, Kalonzo alikwenda ikulu nyakati za usiku wakati wa mkutano wa marais wa Afrika na alimuona akifurahia chakula huku akipiga picha na baadhi ya mawaziri wa serikali ya Kenya Kwanza.

Gachaua alikuwa anahoji ni kwa nini yeye hajafukuzwa kutoka muungano wa Azimio kama ambavyo wabunge kadhaa wa ODM walivyofanyiwa wiki hii baada ya kukutana na rais Ruto katika ikulu ya Nairobi miezi michache iliyopita.

“Raila akija [ikulu] hakuna Makosa, hata juzi tulikuwa ikuluni na Kalonzo alifika. Alikuwa pale, amekuja na giza, mbona hawezi kuja mchana? Niliona Murkomen anapiga picha na huyo mtu, mbona hawajamfukuza yeye kwa Azimio?” Gachagua aliuliza.

“Kama hawa wabunge walikutana na rais wako na makosa, Kalonzo amekuja pale na amekula chakula, amefungwa kitambaa hapa [kiunoni] cheupe amekula vizuri si huyo ndio wa kufukuzwa? Kama watu lazima wafukuzwe kwa kukutana na rais, mbona huyu Kalonzo na alikuwa pale siku tulikuwa na marais wa Afrika na nikaona anafurahia chakula, supu, nini anakaa vizuri kufurahia, iko makosa gani?” aliongeza.

Mapema wiki hii, Odinga aliangusha mjeledi kwa wabunge wa ODM ambao walikutana na Ruto kwa kile alisema kuwa ni kuasi kanuni za chama na hivyo kusisitiza kwamba atasukuma msajili wa vyama kuwaondoa kwenye sajili ya ODM ili kutangaza nyadhifa zao kuwa ziko wasi na hivyo kuandaliwa kwa uchaguzi mwingine.