Naibu wa rais Rigathi Gachagua kwa mara nyingine tena ameelezea kwa ufafanuzi kuhusu kazi yake kuu katika serikali ya Kenya Kwanza.
Gachagua ambaye alikuwa anazungumza Ijumaa alisema kwamab kazi yake kubwa ni kumchunga bosi wake Rais William Ruto dhidi ya kukaribiwa na kinara wa upinzani Raila Odinga, akisema kwamba hana kazi nyingine Zaidi ya hiyo.
Kiongozi huyo alitoa mfano akisema kwamba miezi michache iliyopita alipokwend ziara ya kimataifa nchini Italia, aliambiwa kwamba kuna fununu Odinga ameanza kufanya majaribio ya kumkaribia Ruto na aliitwa na kurudi haraka.
“Sasa alikuwa amejaribu kuja hapo karibu na rais, juzi nimetoka nimeenda ng’ambo nilienda Italia. Walijaribu kupitia huku na kule, nikaitwa nikarudi haraka. Kwa sababu pale unajua kazi yangu pale ni rahisi sana. Kazi yangu ni kuchunga rais William Ruto, sina kazi nyingine. Hiyo ndio kazi yangu. Nikiona mtu yeyote anayeweza kutatiza serikali yake, hiyo ndio kazi yangu kupambana na huyu mtu,” Gachagua alisema.
Gachagua alisema kwamba sasa hivi amepanga kwenda Kolombia na Cuba kuwatafutia wakulima wa Kahawa humu nchini soko.
Alisema kwamba hata hivyo, safari hii amejipanga kwani ameweka mitego kila mahali katika ikulu na hakuna ufanisi wowote kwa Odinga kumfikia rais wakati yeye [Gachagua] atakapokuwa mbali.
“Hiyo ikulu nimeweka mitego kila kona. Nimejipanga. Na niko na watu wa kunipiga simu, wakionekana tu karibu naigiwa simu,” alisema.
Gachagua alisema kwamba historia ya Odinga wanaijua na alimwambia ana kwa ana walipokutana katika mkutano mmoja wa mazishi huko Nyandarua.
“Huyu mzee wa kitendawili [Raila Odinga] amenikuta kwa mazishi juzi hapo Nyandarua, akaniambia ooh wewe mbona hutaki mazungumzo, kubali tufanye mazungumo. Mimi nikaamka nikamwambia mimi siogopi mazungumzo, kile kitu naogopa ni wewe. Kwa sababu pahali pote umeenda umeharibu kutoka kwa Moi, Kibaki na hata kwa Uhuru. Shida yetu na wewe ukikaribia hata Ruto tunaona atapotea. Nilimjibu hapo kwa sababu ni vizuri kuambia mtu ukweli,” Gachagua alisema.