Kama mimi ni kahaba wa kisiasa basi kila aliyekutana na Ruto ni kahaba - Jalang'o

Jalang’o alisisitiza kwamba bado katika uchaguzi wa 2027 atatumia tikiti ya chama cha ODM kurudi tena bungeni kwa muhula wa pili kama mbunge wa Lang’ata.

Muhtasari

• “ODM pengine kama wanapanga kupoteza hiki kiti basi waninyime hiyo tikiti. Mimi nasema tu hapa Lang’ata ni mpaka dakika ya mwisho,” alisema.

MBUNGE WA LANG'ATA
MBUNGE WA LANG'ATA
Image: FACEBOOK

Mbunge wa Lang’ata Phelix Odiwuor maarufu kama Jalang’o amezungumzia kauli ya kiongozi wa chama cha ODM kuwataja wabunge walioasi kanuni za chama kwa kukutana na rais Ruto kama makahaba wa kisiasa.

Jalang’o ambaye alikuwa anazungumza na waandishi wa habari za mitandaoni katika uwanja wa ndege wa Wilson huko Lang’ata wakati wa uzinduzi wa safari za ndege za kampuni ya Skyward kuelekea Migori, alisema kwamba yeye haoni kama kuna kosa lolote alilifanya na wenzake kwa kukutana na Ruto katika ikulu ya Nairobi.

“Katiba inatupa uhuru kwa kujumuika na kukutana na mtu yeyote. Hakuna tatizo kukutana na rais. Ni wanasiasa wangapi wa upinzani ambao wamekutana na rais? Hata Raila Odinga na Kalonzo mwenyewe, magavana wote, wabunge wengi, lakini sasa ikija ni kwa Jalang’o hapo ndio kuna shinda, hilo pekee linaweza kuambia kitu,” Jalang’o alisema.

Alisema kuwa kiongozi wa chama chake cha ODM, Raila Odinga kutumia lugha ya ‘ukahaba wa kisiasa’ ili kuwaelezea wabunge wa ODM waliokutana na rais ikuluni, ni lugha ambayo haina athari yoyote kwake kwani wanasiasa wengi wanatumia lugha ambazo wanaona zina muktadha.

Jalang’o alisema kama kweli yeye na wenzake waliotimuliwa chamani ni makahaba wa kisiasa basi kila mtu aliyekutana na uto vile vile ni kahaba.

“Ni siasa na siasa unaweza tumia lugha yoyote ambayo unadhani inaweza fikisha ujumbe wako kwa hadhira husika. Na kama sisi ni makahaba wa kisiasa basi kila mtu ni kahaba wa kisiasa kwa sababu wote wamekutana na rais. Sasa kila mtu mwenye amekutana na rais wakati mazungumzo ya pande mbili yanaendelea ni msaliti wa chama basi ni hivyo,” aliongeza.

Jalang’o alisisitiza kwamba bado katika uchaguzi wa 2027 atatumia tikiti ya chama cha ODM kurudi tena bungeni kwa muhula wa pili kama mbunge wa Lang’ata.

“ODM pengine kama wanapanga kupoteza hiki kiti basi waninyime hiyo tikiti. Mimi nasema tu hapa Lang’ata ni mpaka dakika ya mwisho,” alisema.