Mhubiri wa Marekani Benny Hinn afichua maelezo ya mkutano wake na Rachel Ruto

"Jambo la kustaajabisha lilifanyika. Mke wa Rais wa Kenya alisafiri kwa ndege kutoka Nairobi na timu yake, kwa sababu moja tu

Muhtasari
  • Mwinjilisti huyo alifichua kwamba Mke wa Rais alimwambia kuwa mkutano huo hautakuwa tu wa nchi nzima bali pia utafadhiliwa kikamilifu na serikali ya Kenya.
  • Mhubiri huyo alisema ilimshangaza kwa vile hakuwahi kupata mke wa Rais kumwalika kwa kampeni iliyofadhiliwa na serikali.

Mhubiri maarufu wa Marekani Benny Hinn amefichua maelezo ya mkutano wake na Mke wa Rais wa Kenya Racheal Ruto.

Alipokuwa akiendesha mojawapo ya mahubiri yake, Mchungaji Hinn alisema kuwa Bi Ruto alisafiri kwa ndege hadi Orlando, Florida, pamoja na timu yake, kumwomba ahudhurie mkutano wa kidini Nairobi.

Mwinjilisti huyo alifichua kwamba Mke wa Rais alimwambia kuwa mkutano huo hautakuwa tu wa nchi nzima bali pia utafadhiliwa kikamilifu na serikali ya Kenya.

"Jambo la kustaajabisha lilifanyika. Mke wa Rais wa Kenya alisafiri kwa ndege kutoka Nairobi na timu yake, kwa sababu moja tu; kuniomba nirudi Nairobi kwa kampeni ya kitaifa iliyofadhiliwa na serikali," Hinn alisema.

Mhubiri huyo alisema ilimshangaza kwa vile hakuwahi kupata mke wa Rais kumwalika kwa kampeni iliyofadhiliwa na serikali.

"Wakati pekee ambao nadhani tumewahi kuwa nayo ilikuwa huko Papua New Guinea," aliongeza.

Hinn alisema Ruto aliandamana na mhubiri wa Uganda Robert Kayanja, kwani walitaka mikutano hiyo ya msalaba ifanyike kwa pamoja nchini Kenya na Uganda.

"Wanataka kufanya mikutano miwili ya msalaba kwa kila nchi, nikasema, Sawa, Bwana, bado una wakati zaidi kwangu," alisema zaidi.

Mke wa Rais anafahamika kuwa ni mtu wa kidini na huandaa maombi Ikulu na maeneo mengine nchini ili kuombea ukame, nchi na hata mumewe.