Video: Seneta wa Kisumu akikata utepe kufungua rasmi 'kibanda' kama ofisi ya naibu chifu

Ofisi hiyo ilikuwa na kuta za mabati na kuezekea paa, ikiwa na mlango wa mbao uliofungwa kwa urahisi na sakafu isiyo na simiti na nyufa zinazoonekana katikati ya ukuta na sakafu.

Muhtasari

• Kwa mujibu wa waliosambaza video hiyo seneta huyo alikuwa akizindua ofisi ya chifu msaidizi wa eneo ndogo la Achego katika Kaunti ya Kisumu.

Profesa Tom Ojienda.
Profesa Tom Ojienda.
Image: Tiktok

Video ikimuonesha seneta wa Kusumu Profesa Tom Ojienda akikata utepe kama njia ya kufungua rasmi nyumba ndogo ya mabati ambayo ilijengwa kama ofisi ya naibu chifu imezua hisia kinzani katika mitandao ya kijamii.

Katika video hiyo, seneta huyo ambaye katika siku za hivi karibuni amekuwa chini ya shinikizo kutoka kwa uongozi wa chama cha ODM kujiuzulu  baada ya kukutana na rais Ruto kinyume na kanuni za chama hicho, alionekana akiwa ameshikilia kipaza sauti katika mkono mmoja huku mkono mwingine ameshikilia mkasi tayari kukata utepe huo uliokuwa umewekwa kwa mlango.

Kwa mujibu wa waliosambaza video hiyo seneta huyo alikuwa akizindua ofisi ya chifu msaidizi wa eneo ndogo la Achego katika Kaunti ya Kisumu.

Hata hivyo, kilichoteka hisia za wanamtandao wengi ni kiwango cha ofisi aliyokuwa akizindua afisa huyo wa serikali.

Ofisi hiyo ilikuwa na kuta za mabati na kuezekea paa, ikiwa na mlango wa mbao uliofungwa kwa urahisi na sakafu isiyo na simiti na nyufa zinazoonekana katikati ya ukuta na sakafu.

"Kuna dalili za maendeleo ambazo unaweza kuziona. Na ndio maana nasema nitasimama na serikali kila wakati kwa sababu serikali ndiyo njia pekee ya kuwaletea maendeleo watu wako," Ojienda alinaswa kwenye video akiwaambia wasikilizaji wake.

Watu katika mitandao ya kijamii hawakuchelewa kumweka kikaangoni wengine wakimuuliza iwapo hayo ndio maendeleo ambayo alidai kwenda kutafutia wananchi wake ikulu wakati wa mkutano wa wabunge ‘waasi’ wa ODM na rais Ruto.