Khalwale akosolewa vikali kwa kutuma Sh200 kwa Mkenya na kubaki na zaidi ya 50,000 kwenye M-pesa

Khalwale alimtumia mwanaume huyo Ksh200 na kubaki na Ksh 51, 385 katika akaunti yake ya M-Pesa.

Muhtasari

•Khalwale alituma Ksh. 200 kwa mtumizi huyo wa Twitter na ili kuthibitisha kitendo chake cha ukarimu, akaonyesha meseji ya M-Pesa kupitia ukurasa wake.

•Huku akimjibu mtumiaji mwingine wa Twitter aliyemwambia kwamba alipaswa kutuma angalau shilingi 1000, alisema, “Kwani Kahawa kikombe ni 1000/-

Dr Boni Khalwale Seneta Kaunti ya Kakamega Picha: Heshima.
Dr Boni Khalwale Seneta Kaunti ya Kakamega Picha: Heshima.
Image: MAKTABA

Seneta wa Kakamega Boniface Khalwale alijipata akijibizana na wanamitandao siku ya  Jumamosi asubuhi baada ya kutuma shilingi 200 pekee kwa Mkenya mmoja ambaye alikuwa amemwomba amnunulie kikombe cha kahawa.

Mtumiaji wa Twitter kwa jina Gichane Anthony alikuwa ametumia mtandao huo wa kijamii kumuomba seneta huyo wa UDA amnunulie kikombe cha kahawa Jumamosi asubuhi,  leo ikiwa ni wikendi.

“Habari za asubuhi Seneta Boni.. Leo ikiwa ni wikendi, nitafurahi ukininunulia kikombe cha kahawa. Asante mapema, Bwana Seneta,” Gichane aliandika chini ya moja ya machapisho  ya seneta huyo kwenye Twitter na kutoa nambari yake ya M-Pesa.

Khalwale alikubali ombi hilo kwa nia njema na kutuma Ksh. 200 kwa mtumizi huyo wa Twitter na kwa kuthibitisha kitendo chake cha ukarimu, akaonyesha meseji ya M-Pesa kupitia ukurasa wake.

Maelezo ya meseji yalionyesha kuwa mwanasiasa huyo alituma shilingi 200 kwa mwanamume huyo saa mwendo wa saa kumi na moja na dakika hamsini asubuhi ya  Jumamosi na kubaki na Ksh 51, 385 katika akaunti yake ya M-Pesa. Hili lilizua hisia mseto kutoka kwa wanamitandao huku wengi wakimkosoa na wengine wakijitokeza kumtetea.

Image: SCREENSHOT// TWITTER

@kombulu alimwambia, “Napenda mtindo wako wa uongozi na wewe ni mfano wa kuigwa kwangu lakini kwenye hili natofautiana na wewe. Unathubutuje kutumia mtu mzima Ksh 200 kwa kikombe cha chai hakika. Angalau ungemtumia 2k. Umeniangusha.”

Khalwale akajibu, “Kama unataka nikutumie 2k, sema tu."

@kabiadow alisema, "Nunua chai inamaanisha kutuma angalau 1,000."

Akajibu, “Hakusema chai. Alisema kahawa!"

Huku akimjibu mtumiaji mwingine wa Twitter aliyemwambia kwamba alipaswa kutuma angalau shilingi 1000, alisema, “Kwani Kahawa kikombe ni 1000/-”

Hata kama wanamitandao kadhaa wakimkosoa, baadhi yao walionekana kukubaliana na kitendo chake na kumtetea vikali.

@254Chrome alisema, “Sasa mnataka chai ya elfu kumi.. hata angetuma chwani.”

@TheeBilly: Ksh 200 inatosha kwa alichoomba. Sioni kwanini watu wanalalamika.

@SaidYuske44930 Uko sahihi kabisa. Hicho ndicho kinachoombwa kwa kipindi hiki.

@cursedsperm_1 Kuna watu wanapotokshwa, kahawa maana yake kahawa.. kahawa sio chai.