Utamaduni Dei: Jinsi Kuria alitokea na vazi la kitamaduni la kumruhusu kuoa wanawake wengi

“Najua sasa vile mumeniona, pahali nimetoka, niko na mamlaka yote ya kutangaza Amani, kutangaza vita na kuoa wanawake wengi." Moses Kuria alisema.

Muhtasari

• Kuria pia aliweza kuelezea umuhimu wa siku ya Utamaduni ambayo wengi wa Wakenya huisi kama si ya umuhimu wowote nchini.

Moses Kuria
Moses Kuria
Image: X

Octoba 10 nchini Kenya ni siku ya mapumziko ambayo inawapa Wakenya fursa ya kusherehekea na kufurahia utamaduni wao.

Ni siku ambayo awali kabla ya kubadilishwa ilikuwa inaitwa Moi Dei.

Mwaka huu, sherehe za Utamaduni Dei ziliadhimishwa katika ukumbi wa Bomas jijini Nairobi na ziliongozwa na mama wa taifa, Bi Rachel Ruto na  baadhi ya viongozi wa serikali akiwemo waziri wa huduma za umma Moses Kuria na mkuu wa utumishi wa umma Felix Kosgei miongoni mwa wengine.

Kilichowazuzua wengi ni mavazi ambayo viongozi hao walivalia katika sherehe hizo.

Kando na vazi la bei ghali alilotoka nalo mama wa taifa, Moses Kuria naye alizua mjadala na minong’ono mitandaoni baada ya kutokea na vazi la kitamaduni la jamii ya Agikuyu.

Kuria alijikokote kwenda jukwaani akiwa amevalia vazi hilo na aliweza kutoa maelezo kiasi kuhusu vazi lenyewe huku pia akiwaomba Wakenya kutangamana katika utamaduni wao.

Kuria alieleza kwamba vazi hilo la kitamaduni pindi anapolivalia moja kwa moja humpa kibali cha kutangaza Amani, vita na hata ruhusa ya kuoa wanawake wengi.

“Najua sasa vile mumeniona, pahali nimetoka, niko na mamlaka yote ya kutangaza Amani, kutangaza vita na kuoa wanawake wengi. Na ndio maana nimepewa mamlaka hayo na katiba ya kule ninakotoka,” Kuria alisema katika hotuba yake iliyojawa na mbwembwe.

Kuria pia aliweza kuelezea umuhimu wa siku ya Utamaduni ambayo wengi wa Wakenya huisi kama si ya umuhimu wowote nchini.

“Sababu kuu ambayo tunasherehekea na kuadhimisha siku hii kama Utamaduni Dei ni kupiga tathmini kama nchi kwanza kule tumetoka, na pili kule tunakoenda kama wananchi, wakati naangalia kwa sisi tulioko hapa leo, tuna mengi ambayo tunaweza jifunza kutoka kwa utamaduni na mila zetu,” Kuria alisema.