Katibu wa COTU Francis Atwoli asema watasimama na wakili feki Brian Mwenda

"COTU (K) ingependa kumfahamisha Brian Njagi kwamba tunapatikana na tuko tayari kumuunga mkono ili kuhakikisha ndoto zake zinatimizwa," Atwoli alimtetea.

Muhtasari

• "Shirika Kuu la Vyama vya Wafanyakazi (Kenya), COTU (K), linapenda kueleza uungaji mkono wake mkubwa kwa Brian Mwenda," Atwoli alisema.

COTU kusimama na Brian Mwenda, wakili feki.
COTU kusimama na Brian Mwenda, wakili feki.
Image: Facebook

Katibu mkuu wa muungano wa wafanyikazi nchini Francis Atwoli amesema kwamba muungano huo utasimama na Brian Mwenda, jamaa aliyetumbuliwa kuwa wakili feki na chama cha wanasheria Kenya, LSK jijini Nairobi.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Atwoli alichapisha notisi akisema kwamba watasimama upande wa uetetzi wa wakili huyo feki ambaye alisemekana kushinda kesi 26 kati ya zile ambazo aliwawakilisha watu mbali mbali kwenye mahakama nchini.

Alidai kuwa Mwenda ambaye amekuwa akifanya kazi za sheria na kuwawakilisha wateja kwa mafanikio, anapaswa kufanyiwa uchunguzi wa haki na wa uwazi ili kupima ujuzi na umahiri wake.

"Shirika Kuu la Vyama vya Wafanyakazi (Kenya), COTU (K), linapenda kueleza uungaji mkono wake mkubwa kwa Brian Mwenda Njagi, Mkenya kijana na mahiri ambaye hivi majuzi amelaaniwa kwa kutekeleza sheria bila sifa za kisheria," Atwoli alisema.

"COTU (K) ingependa kumfahamisha Brian Njagi kwamba tunapatikana na tuko tayari kumuunga mkono ili kuhakikisha ndoto zake zinatimizwa," kiongozi wa leba alimtetea Mwenda, ambaye hadithi yake ilizua hisia tofauti nchini kote.

Katika taarifa yake, Atwoli alidai kuwa anafahamu wataalamu kutoka sekta mbalimbali ambao walikuwa wakifanya mazoezi bila karatasi zinazohitajika. Mwenda, alionya hivyo, asitolewe kafara au kutumiwa kama mbuzi wa kafara.

"Kama kiongozi mwenye uzoefu wa kazi, naweza kusema kwa uthabiti kwamba kesi ya Brian sio ya kipekee. Najua wahandisi wengi wakubwa, wahasibu, walimu, wataalam wa IT, wataalam wa usalama wa mtandao, wafanyikazi wa kijamii, wabunifu, wanasoka, wakulima, wahamiaji, mafundi bomba, mafundi seremala, na wahudumu wa afya ambao ni wataalamu katika maeneo wanayopenda lakini bila karatasi yoyote ya kuonyesha sifa zao.”

"Wakati baadhi yao huvumilia maumivu ya kuwa darasani ili kufundishwa kile ambacho tayari wanakijua, wengi hawakijui na hivyo kuishia kubaguliwa," alionya.