Kijana wa miaka 20 ajinyonga kwa kukosa nauli kwenda kumzika baba mkwe

“Mume wangu alikufa tatizo lilikuwa ni kukosa hela ya nauli ya kwenda msiba nyumbani kwetu." Mkewe marehemu ambaye pia alikuwa anaomboleza kifo cha babake alieleza.

Muhtasari

• Alisema kwamba msiba ulitokea kwao na awali waliketi na mumewe wakazungumza na kukubaliana kwamba amekosa hela ya kufanya nauli kwenda msiba ukweni.

Image: Hisani

Kijana mmoja aliyefahamika kwa jina William Bahati mwenye umri wa miaka 20 mkazi wa mkoa wa Geita nchini Tanzania ameripotiwa kujitia kitanzi kwa kutumia Kamba ya mbuzi huku sababu zikitajwa ni kukosekana kwa nauli ya kwenda ukweni.

Kwa mujibu wa mkewe, Grace Jeremiah, kijana huyo alitaabika kupata nauli ya kwenda ukweni kwa ajili ya msiba wa baba mkwe – ambaye ni babake mke wake huyo aliyesimulia tukio hilo.

“Mume wangu alikufa tatizo lilikuwa ni kukosa hela ya nauli ya kwenda msiba nyumbani kwetu. Nilikuwa ndani, ilikuwa saa kumi na moja, aliamka akavaa nguo akatoka akisema anaenda shambani. Baadae tukamkuta hapo amejinyonga,” Mkewe marehemu alisimulia.

Alisema kwamba msiba ulitokea kwao na awali waliketi na mumewe wakazungumza na kukubaliana kwamba amekosa hela ya kufanya nauli kwenda msiba ukweni.

“Sasa sijui alipatwa na huo huzuni wa kukosa nauli ndio akafanya uamuzi wa kujinyonga,” Bi Grace alisema.

Mwenyekiti wa kijiji hicho alisema kwamba ni kweli tukio hilo lilitokea na kuwataka vijana kutochukua uamuzi mgumu wa kujitoa uhai.

Alisema kwamba limekuwa ni jambo la kawaida kwa nchi kupoteza vijana wengi ambao ni nguvu kazi ya taifa kwa njia ya kiholela huku akitoa wito kwa vijana kufanya mazungumzo na watu ili kueleza matatizo yanayowakumba kupata ufumbuzi badala ya kujinyonga.