Moses Kuria ashutumu polisi kumhangaisha gavana wa Meru Kawira Mwangaza

Kuria alishtumu serikali anayoihudumia kumhangaisha Mwangaza njia sawa na ile serikali iliyopita ya Uhuru Kenyatta ilivyowahangaisha wale walioegemea mrengo wa Ruto.

Muhtasari

• “Ni makosa kumnyanyasa Gavana Kawira Mwangaza sawa sawa na serikali nyingine ilivyokuwa ikitunyanyasa baadhi yetu,” Moses Kuria alidai.

Kawira Mwangaza
Kawira Mwangaza
Image: X//screengrab

Waziri wa huduma za umma Moses Kuria amewashtumu polisi kwa kile anasema wanamhangaisha gavana wa Meru Kawira Mwangaza kwa njia isiyostahiki hata kidogo.

Mwangaza Jumatano alasiri alipakia picha na video kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii akionesha jinsi maafisa wa polisi walivamia na kusambaratisha mkutano wake ambao alikuwa ameandaa katika kuendeleza mradi wake wa ‘Okolea Jamii’ – mradi ambao ni wa kutoa ng’ombe wa maziwa kwa wakazi wa kaunti hiyo.

Akiwa anawahutubia watu, maafisa wa polisi walifika na kumtaka kujongea pembeni kuzungumza naye kabla ya kuwaambia wananchi kila mmoja kuondoka huku wakisema kwamba mkutano huo ni haramu na hauna kibali cha kuandaliwa.

Baadae waliandamana na Mwangaza hadi kwenye gari la polisi lililokuwa limesubiri lakini baadae idara ya polisi ikakanusha madai kwamba walimkamata huku wakigeuza hafithi kuwa kwamba gavana huyo ndiye aliyejiingiza kwenye gari la polisi kwa hiari akidai ametiwa mbaroni.

Hatua hiyo imemkasirisha waziri Moses Kuria akidai kwamab kuhangaishwa kwa Mwangaza na serikali anayoihudumia hakuna tofauti na jinsi serikali iliyopita ya Uhuru Kenyatta ilivyokuwa ikiwahangaisha wale walioonekana kuegemea mrengo wa Ruto kipindi hicho akiwa naibu rais.

“Ni makosa kumnyanyasa Gavana Kawira Mwangaza sawa sawa na serikali nyingine ilivyokuwa ikitunyanyasa baadhi yetu,” Moses Kuria alidai.

Itakumbukwa gavana Mwangaza kando na kuwa amekuwa akizozana na MCAs wa kaunti hiyo ambao wanataka kuandaa hoja ya kumbandua madarakani kwa mara ya pili, pia amekuwa akizozana na waziri wa usalama wa ndani profesa Kithure Kindiki ambaye wiki chache zilizopita alipiga marufuku mkutano wowote wa Mwangaza wa ‘Okolea Jamii’ akidai kwamba mikutano yake husababisha fujo.