Utahitaji mboni ya jicho tu ili kutoa na kutuma pesa kwa simu na benki kuanzia Desemba

"Wakenya wataweza kutambuliwa kwa njia ya kidijitali kwa kutumia mboni za macho au alama za vidole na tunaweza kufanya miamala bila hitaji la watu kuhangaika kujitambulisha."

Muhtasari

• Mnamo Septemba, serikali iliahirisha uzinduzi uliopangwa kutokana na hali zisizoweza kuepukika na kuahidi kutangaza tarehe mpya.

Ruto
Ruto
Image: Facebook

Wakenya wa matabaka yote sasa watahitaji tu mboni za macho na alama za vidole ili kufanikisha shughuli za utoaji na kutuma pesa kwa njia ya simu au benki kuanzia mwezi Desemba, rais Ruto amesema.

Rais Ruto akizungumza Jumatatu, alisema kwamba uongozi wake unaendelea katika jitihada za kupiga hatua kuhamisha shughuli nyingi kwenye mifumo ya kidijitali na kwamba kadi ya kidijitali ya Maisha Namba itakwua inarahisisha shughuli zote za miamala.

Rais aliahidi kwamba Kitambulisho cha Dijitali kitaanza kutumika Desemba na programu ya majaribio itakamilika mwishoni mwa Novemba ili kufungua njia kwa uzinduzi huo bila mshono.

Mnamo Septemba, serikali iliahirisha uzinduzi uliopangwa kutokana na hali zisizoweza kuepukika na kuahidi kutangaza tarehe mpya.

"Nimehakikishiwa na washikadau wote wakiongozwa na Wizara zinazohusika kwamba kufikia Desemba tutaweza kuzindua vitambulisho vya kidijitali ambapo kila Mkenya hatalazimika kubeba plastiki yoyote ya karatasi au vinginevyo kama kitambulisho," akasema.

Rais Ruto alisema kuwa utekelezwaji uliopangwa ulikuwa uko mbioni akisema kuanza kwa utumizi wa kitambulisho cha kitaifa kinaendelea.

"Wakenya wataweza kutambuliwa kwa njia ya kidijitali kwa kutumia mboni za macho au alama za vidole na tunaweza kufanya miamala bila hitaji la watu kuhangaika kujitambulisha wao ni nani," Rais alibainisha.

Kikiwekwa kuchukua nafasi ya vitambulisho vya sasa vya kitaifa, kitambulisho kilichowekwa kidijitali kitajumuisha data zote za kina za kitambulisho ikiwa ni pamoja na Cheti cha Kuzaliwa, cheti cha kifo, kadi ya Maisha pamoja na leseni ya udereva miongoni mwa vingine.

Watoto wachanga watapewa nambari tofauti ambayo itatumika kama nambari ya cheti cha kuzaliwa na baadaye kama nambari ya utambulisho kwa huduma zote za serikali, ikijumuisha, usajili wa kifo.

 Kwa upande mwingine, Kitambulisho cha Dijitali kitakuwa uwakilishi wa kidijitali wa mtu binafsi, shirika au kifaa, kwa kawaida kikijumuisha sifa za kibinafsi, vitambulisho na uthibitishaji.

Uboreshaji huu unatofautisha Maisha Card na mtangulizi wake, Huduma Card, ambayo iliashiria jaribio la kuweka utambulisho wa kidijitali chini ya utawala wa Rais wa zamani Uhuru Kenyatta.