Nyeri: Kundi la nyuki lazuka kituo cha matatu na kushambulia magari ya sacco moja pekee

Baadhi walihisi ni ushirikina lakini wengine wakikanusha dhana hiyo wakisema nyuki walikuwa tu katika harakati zao za kutafuta mzinga.

Muhtasari

• “Nyuki wanaozagaa wakitafuta tu nyumba mpya (Mzinga). Imani za kichaa hutokea Afrika pekee,” Steffano Gizzler alisema.

Nyuki
Nyuki
Image: Screengrab

Kizaazaa kilishuhudiwa katika stendi kuu ya magari ya uchukuzi wa umma mjini Nyeri baada ya pumba la nyuki kuzuka na kuzagaa huku wakizingira matatu ya sacco moja tu kati ya sacco kadhaa yaliyokuwepo kwenye kituo hicho.

Kwa mujibu wa video ambazo zimesagaa mitandaoni, nyuki hao wengi walilazimisha biashara kusambaratika kila mmoja akisimama kando kutazama tukio hilo lisilo la kawaida.

Wakazi walisema kwamba nyuki hao walifurika na kuanza kuzingira magari ya sacco hiyo moja tu huku gari la sacco nyingine likiingia wala nyuki hawalikaribii lakini gari la kutoka sacco sawia na hiyo likiingia nyuki wanalizingira.

Hata hivyo, tukio hilo lilivutia maoni kinzani baadhi wakisema kwamba hakuna kubwa Zaidi ya nyuki kutafuta sehemu mpya ya kujikita na wengine wakihusisha tukio hilo na ushirikina.

“Nyuki wanaozagaa wakitafuta tu nyumba mpya (Mzinga). Imani za kichaa hutokea Afrika pekee,” Steffano Gizzler alisema.

“Kwani mwenyewe alikataa kulipa mikopo wenye kumsimamia kulipa wakakasirika ama ni wivu ya kibiashara,” Karend Kitchen aliuliza.

“Rudisheni vitu za wenyewe! There must be something,” Gabby Wainaina aliongeza.

“Waa mimi naogopa kuona Mambo kama haya,” Eddah Wekesa alionesha wasiwasi wake.

Tazama video hii jinsi nyuki hao walizua wasiwasi baina ya wahudumu wa matatu hizo na abiria.