Dereva wa basi akamatwa kwa kosa la kuendesha huku akichat WhatsApp

Jemba alirekodiwa kwa siri na abiria akituma ujumbe mfupi na kuperuzi kupitia simu yake ya mkononi wakati akishuka kwa kasi kwenye barabara kuu.

Muhtasari

• Katika video hiyo, dereva huyo alionekana amekita macho yake katika kiwambo cha simu yake huku akiwa anaendesha pasi na kuwa makini barabarani.

Dereva anachat
Dereva anachat
Image: Screengrab

Dereva wa basi aliyeonekana kwenye video iliyoenda viral akiwa bize kuchat huku akiwa anaendesha basi la abiria kwa kasi hatimaye ameripotiwa kutiwa mbaroni.

Dereva huyo wa basi la Link nchini Uganda alinaswa kwenye video na mtu anayekisiwa kuwa mmoja wa abiria aliyekaa katika kiti cha mbele pembezo ni mwake.

Katika video hiyo, dereva huyo alionekana amekita macho yake katika kiwambo cha simu yake huku akiwa anaendesha pasi na kuwa makini barabarani.

Mtuhumiwa huyo alitambuliwa kama Andrew Jemba (43) ambaye ni dereva wa basi hilo lenye namba za usajili UBG 188P, mali ya Kampuni ya Link Bus Services.

Jemba alirekodiwa kwa siri na abiria akituma ujumbe mfupi na kuperuzi kupitia simu yake ya mkononi wakati akishuka kwa kasi kwenye barabara kuu ya Kampala - Fortportal.

Video hiyo ambayo ilisambaa mitandaoni Jumanne na Jumatano ililaaniwa vikali na watumiaji wa mitandao ya kijamii, huku wengi wao wakitaka akamatwe.

Majira ya saa sita asubuhi siku ya Jumatano, Polisi walifanikiwa kumkamata dereva huyo na kumzuilia katika Kituo cha Polisi cha Kyegegwa, vyombo vya habari nchini humo viliripoti.

"Polisi kwa hiyo wanawapongeza wananchi kwa umakini wao juu ya usalama barabarani na kutoa wito kwa kila mtu kuendelea kuripoti na kutoa taarifa zozote za ukiukwaji wa sheria za barabarani kwenye nambari yetu ya bure 0800199099," polisi walinukuliwa wakisema baada ya kufanikiwa kukamatwa kwa dereva huyo.

"Tunaendelea kutoa onyo kwa madereva wote wanaotumia simu wakati wa kuendesha gari kwani hii imeonekana kuwa moja ya sababu za ajali za barabarani nchini."